Kessy kubaki Simba, Yanga basi tena

09Mar 2016
Lasteck Alfred
Dar
Lete Raha
Kessy kubaki Simba, Yanga basi tena

BAADA ya kuwa na tetesi za hapa na pale kuwa beki wa kulia wa Simba, Hassan Kessy huenda akatua Yanga, menejimenti ya mchezaji huyo imethibitisha kuwa mchezaji huyo anaenda Ulaya kucheza soka la kulipwa na kama haitakuwa hivyo basi atabaki Simba.

Hassan Kessy.

Meneja wa beki huyo, Athumani Tippo ‘Zizou’, alisema, “Kwasasa niko Dubai, kwaajili ya shughuli zangu binafsi, lakini kiufupi tulifanya mazungumzo na klabu ya Simba na kuafikiana kuwa Kessy ataendelea kukipiga kwenye klabu hiyo.

“Kwenye makubaliano yetu na klabu hiyo ni kuwa Kessy atasaini mkataba baada ya msimu kumalizika na si sasa hivi kwasababu kuna timu ambayo anatakiwa kwenda kufanya majaribio Ulaya na kama atafanikiwa basi atauzwa kama mchezaji huru, kama atashindwa majaribio basi nafasi itakuwa ni kwa Simba pekee kumpa mkataba mpya,” alisema Tippo.

Hata hivyo, meneja huyo ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa Coastal Union, alisema kuwa hawajapokea rasmi ofa ya Yanga hivyo taarifa ambazo kimekuwa zikizagaa kuwa beki huyo anaondoka si za kweli.

Simba ilimsajili Kessy kipindi cha dirisha dogo la usajili Desemba 2014 kwa mkataba wa miezi 18.