Mkwasa aita wachezaji 25 kuivaa Chad

09Mar 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe
Mkwasa aita wachezaji 25 kuivaa Chad

MSHAMBULIAJI Mbwana Samatta atavaa beji ya unahodha wa Timu ya Taifa (Taifa Stars) kwa mara ya kwanza tangu alipopewa jukumu hilo pale atakapowaongoza wenzake kuivaa Chad katika mechi ya kuwania kufuzu kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika.

BONIFACE MKWASSA

Samatta, anayecheza soka la kulipwa na klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji, atabeba jukumu hilo baada ya jana kutangazwa kuwa miongoni mwa wachezaji 25 wa kuunda Taifa Stars, huku nahodha wa zamani, Nadir Haroub 'Cannavaro' na mshambuliaji Mrisho Ngassa anayekipiga Afrika Kusini wakiachwa kutokana na kuwa majeruhi.

Mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa Machi 23 mwaka huu, kisha marudiano Machi 28 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika orodha ya wachezaji hao, Kocha Boniface Mkwasa, amewarejesha kikosini Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude wa Simba na Erasto Nyoni (Azam FC) baada ya kuvutiwa na viwango vyao kwenye mechi za ligi.

Mkwasa alisema uteuzi wake umezingatia utayari wa wachezaji kwa vile hakutakuwa na muda wa kutosha kufanya mazoezi ya pamoja kabla ya mechi.

Aliwataka wachezaji aliowaita katika kikosi hicho kuongeza bidii mazoezini na kujenga nidhamu ya kimchezo.
Kuhusu Samatta na mshambuliaji wa TP Mazembe ya DRC, Thomas Ulimwengu wataungana na timu hiyo Chad na kikosi chake kitaondoka jijini kwa awamu mbili.

Waliotwa kuunda Stars ni Aishi Manula, Ally Mustafa 'Barthez', Shomary Kapombe, Mwinyi Hajji, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Juma Abdul, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni, David Mwantika, Ismail Issa, Jonas Mkude, Himid Mao, Mwinyi Kazimoto na Mohamed Ibrahim.

Wengine; Shiza Kichuya, Farid Mussa, John Bocco, Elius Maguli, Ibrahim Ajib, Deus Kaseke, Said Ndemla, Jeremiah Juma na Shabani Kado.