Mei 10, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, wakihitaji sare au kufungwa bao lisilozidi moja, itaporudiana dhidi ya Marumo Gallants nchini Afrika Kusini.
Yanga itashuka kwenye Uwanja wa Royal Bafokeng nchini Afrika Kusini, saa 1:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki kucheza mechi hiyo ya mkondo wa pili ya hatua ya nusu fainali ambayo itaamua hatma ya timu zote mbili, huku ikipania kuweka rekodi iliyowekwa mwaka 1993 na Simba ambayo ilifanya hivyo wakati huo likiitwa Kombe la CAF kwa kuifunga Atletico Sport Aviacao ya Angola jumla ya mabao 3-1, iliyoshinda kwenye mechi ya kwanza Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) na kwenda kusuluhu ugenini.
Pia, Yanga itakuwa imeweka rekodi ya kutinga fainali kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo iliyoanzishwa mwaka 1935 jijini Dar es Salaam.
Kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, amesema amekiweka tayari kikosi chake kwa ajili ya mechi hiyo ngumu, huku akili yake kubwa ikiwa ni kulinda kile ambacho imekipata nchini kwenye mechi ya kwanza.
Alisema kwa jinsi aliivyoitazama Marumo Gallants si timu ya kubeza na kwa sababu tayari wameshapata ushindi wa mabao 2-0 nyumbani, kikubwa kwao atakachofanya ni kuulinda kwa gharama yoyote, ikiwa ni pamoja na kuwashtukiza wageni kwa bao la ugenini ambalo anadhani litawachanganya na kuifanya mechi kuwa ngumu kwa Wasauzi hao.
"Mechi haitokuwa rahisi kwa sababu wapinzani wetu wana timu nzuri, lakini wana mapungufu yao pia ambayo kama tutayatumia vema tunaweza kufanikiwa katika hili. Wana safu nzuri sana mbele sehemu ya ushambuliaji, hivyo mabeki nimewataka kuwa makini sana, lakini wana shida sehemu ya ulinzi na huo ndiyo mtaji wetu mkubwa kuelekea kwenye mechi hii kwani tunahitaji kuwashtukiza kwa kupata bao moja ili kuvuruga mipango yao yote," alisema Mtunisia huyo.
Katika hatua nyingine, uongozi wa klabu hiyo umesema umepanga kufanya usajili mzito wa kung'oa mmoja kati ya washambuliaji hatari kwenye Ligi Kuu ya Afrika Kusini kwa ajili ya kufanya vizuri zaidi kimataifa na Ligi Kuu msimu ujao.
Taarifa zilizolifikia Nipashe jana kutoka kwa mmoja wa viongozi wa timu hiyo, zimeeleza licha ya kuwa na mchezo mgumu wa hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho, pia wanapambana kuhakikisha wananasa mmoja kati ya washambuliaji hatari katika ligi ya nchi hiyo.
Katika ligi ya Afrika Kusini washambuliaji hatari zaidi ni Mnamibia Peter Shalulile wa Mamelod Sundowns mwenye mabao 12 sawa na Khanyisa Mayo wa Cape Town City.
"Ni kweli uongozi moja ya malengo yake ni kuona unafanikiwa kupata mshambuliaji mmoja mkubwa kutoka hapa Afrika Kusini kwa ajili ya msimu ujao. Hata rais Injinia Hersi Said, ameshatoa muongozo na mipango yake kuwa yupo kwenye jitihada hizo kuona Yanga inafanikiwa kushusha mshambuliaji kutoka Afrika Kusini na ameeleza kwenye mahojiano yake na mwandishi nguli wa Afrika Kusini, Robert Marawa, " alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Mkuu wa Idara ya Habari ya Yanga, Ali Kamwe, alikiri kuwapo kwa mpango huo huku akishindwa kuweka wazi ni mshambuliaji kutoka timu gani kati ya wanaowawania.
"Ni kweli huo mpango upo, lakini ninachoweza kusema ni wale ambao wanapambana katika orodha ya wafungaji wakiwa na mabao sawa japo kuwa kwa sasa mipango yetu ipo kwanza kwenye mchezo wa kesho (leo)," alisema Kamwe.










