Maafande wa JKT Queens ndiyo kwa kiasi kikubwa wanatabiriwa kutwaa ubingwa kutokana na kucheza mechi yao dhidi ya timu dhaifu inayoshika mkia, Mkwawa Queens, mechi itakayofanyika Uwanja wa Samora, Iringa.
Mabingwa wa ligi hiyo kwa misimu mitatu mfululizo, Simba Queens, nao watakuwa huko huko Iringa kucheza dhidi ya Ceasiaa Queens, mechi ikipigwa Uwanja wa Chuo Kikuu cha Mkwawa.
Kwa maana hiyo timu hizo mbili, JKT Queens na Simba Queens, ambazo zipo katika nafasi ya juu zikichuana kutwaa ubingwa msimu huu, zote zitakuwa mkoani humo, hivyo msimu huu bingwa atajulikana akiwa Iringa.
JKT Queens inaongoza kwa kuwa na pointi 43, hivyo ikishinda itafikisha pointi 46 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote.
Simba Queens inachoombea ni maafande hao wafungwe au kutoka sare na wao kushinda, kitu ambacho ni kigumu kutokana na ubora wa JKT Queens na udhaifu wa timu inayocheza nayo ambayo inaburuza mkia ikiwa na pointi tatu tu.
Ili Simba Queens iwe bingwa, inapaswa JKT Queens ifungwe au kutoka sare na yenyewe iibuke na ushindi dhidi ya Ceasiaa Queens, vinginevyo hata ikishinda itafikisha pointi 45 ambazo maafande watakuwa wamezipita wakishinda mechi ya mwisho.
Kocha Mkuu wa Simba Queens, Charles Lukula, pamoja na kukubali lolote litakalotokea, ameshauri kuwapo na michuano mingine kama Kombe la FA ili kuwapa nafasi wachezaji wa kike kucheza mechi nyingi tofauti na sasa ambapo ligi ina timu 10 tu, zikichezwa mechi 18 pekee.
"Ligi ya Tanzania ni ngumu na nzuri, imekusanya wachezaji wazuri wa ndani na nje, ninachoshauri ni kuongezwa kwa timu kidogo kwenye ligi hii, pia kuwe na michuano mingine kama ya Kombe la FA, ili hawa watoto wa kike wawe na muda mrefu wa kucheza," alisema.
Ligi hiyo inatamatika leo kwa mechi zingine kuchezwa Uwanja wa Nyamagana, Mwanza, baina ya Alliance Queens na Baobab Queens, Fountain Gate Princess dhidi ya The Tigers Queens kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma, na katika Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi, Amani Queens itaikaribisha Yanga Princess.










