Shikangwa mfungaji bora Ligi ya Wanawake 2022/23

19May 2023
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Shikangwa mfungaji bora Ligi ya Wanawake 2022/23

WAKATI JKT Queens ikitwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara kwa msimu wa 2022/2023, straika wa Simba Queens, Jentrix Shikangwa ameibuka Mfungaji Bora baada ya kupachika mabao 17.

 

Straika huyo raia wa Kenya alihitimisha hesabu zake kwa kufunga bao pekee kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha Mkwawa, Iringa timu yake ilipocheza dhidi ya wenyeji Mkwawa Queens.

Shikangwa ambaye alisajiliwa katika dirisha dogo la usajili Desemba, mwaka jana amekuwa msaada mkubwa kwenye timu yake iliyomaliza nafasi ya pili baada ya kufikisha pointi 45, moja pungufu dhidi ya mabingwa, JKT Queens.

Mchezaji huyo anafuatiwa na Winfrida Charles wa Alliance Girls ya Mwanza ambaye amefunga mabao 13, Donisia Minja wa JKT Queens mwenye mabao 12 anashika nafasi ya tatu akifuatiwa na Stumai Abdallah wa JKT Queens pia mwenye magoli 10.

JKT Queens ilimaliza ligi hiyo yenye timu 10 kwa kishindo, ikiisasambua Mkwawa Queens mabao 7-2 kwenye mechi iliyochezwa Uwanja wa Samora, mjini Iringa.

JKT Queens inachukua ubingwa huo na kumaliza utawala wa Simba Queens ambayo iliuhodhi kwa misimu mitatu mfululizo.

Ilikuwa inahitaji ushindi tu kwenye mechi hiyo dhidi ya timu dhaifu, Mkwawa Queens iliyoshuka daraja.

Kwa ubingwa huo, sasa itaiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) itakayochezwa kuanzia Juni 3 hadi 17, mwaka huu huko Kenya ili kusaka mwakilishi wa ukanda huu atakayekwenda katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba Queens imeukosa ubingwa kwa kushindwa kuifunga JKT Queens msimu huu, mechi ya kwanza ambayo ndiyo imewaathiri ilifungwa mabao 2-1, kwenye Uwanja wa Mo Arena, Desemba 6, mwaka jana ambayo ilikuwa ni ya ufunguzi wa ligi na Machi 10, mwaka huu waliporudiana, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 , mechi ikichezwa Uwanja wa Meja Jenerali, Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.