Rais Samia aipa ndege Yanga

19May 2023
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Rais Samia aipa ndege Yanga

WAKATI Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan ameipongeza Yanga kwa kutinga fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, kiongozi huyo mkuu pia ametoa ndege kwa ajili ya kuipeleka timu hiyo Algeria katika mechi ya marudiano dhidi ya wenyeji, USMA Alger itakayochezwa

 

Yanga itacheza mechi yake ya kwanza ya hatua ya fainali Mei 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Rais Samia alisema jana ndege hiyo itawasubiri wachezaji, viongozi na baadhi ya mashabiki wa Yanga watakaosafiri katika mechi hiyo ya mkondo wa pili na amewatakia ushindi.

Pia kiongozi huyo namba moja Tanzania  ameahidi kutoa Sh. milioni 20 kama itafanikiwa kushinda mechi ambayo itaipa timu hiyo ushindi.

 "Sasa Yanga inakwenda kwenye fainali, tunapokwenda fainali ni Sh. milioni 20 kama timu ikitoka na ushindi, hii haitakwenda kafungwa mbili, kafunga moja hapana, yawe magoli yote yameipa timu hii ushindi, kila goli milioni 20, lakini zaidi ya hapo, serikali itatoa ndege kuwapeleka katika mchezo wa fainali," alisema Rais Samia jijini jana.

Aliongeza hatua ambayo Yanga imefika ni kubwa na imeiletea nchi heshima.

"Pongezi za dhati kwa klabu ya Yanga kwa kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho (CAF Confederation Cup). Mmeandika historia na kuipa nchi yetu heshima kubwa sana. Nawatakia kila la kheri katika mchezo wenu wa fainali," aliandika rais huyo.

Naye Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, ameipongeza Yanga kwa kutinga fainali, ikiwa ni kwa mara ya pili nchi ikiingia hatua hiyo baada ya miaka 30.

Karia alisema anatamani kuona kiongozi wa Algeria naye akabidhi kombe la ubingwa kwa wageni kama Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, alivyowakabidhi Stella Abidjan ya Ivory Coast iliposhinda dhidi ya Simba, katika mechi ya fainali iliyochezwa  Tanzania.

"Nitumie nafasi hii kuwapongeza Yanga, naamini mwaka huu, sisi tutacheza hapa tutawafunga, tutakwenda kwao, kiongozi wa Algeria atawapa kombe Yanga, kama ambavyo lilichukuliwa hapa, na sisi tutalichukua kwao," alisema Karia.

Rais wa Heshima wa Simba, Mohamed Dewji 'Mo' aliandika kwenye mtandao wake wa 'Twitter' kuipongeza Yanga kwa mafanikio waliyopata.

"Hongera sana mtani, umefanya Tanzania ijivunie." Aliandika Dewji.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze, alisema wamefanya kazi kubwa na wamestahili kufika hapo na sasa wanapaswa kumalizia pale walipoishia.

"Ni faraja kubwa sana, msimu ulikuwa mrefu na tumefanya kazi sana, tumestahili kufika hapa, ila sasa tunapaswa kumalizia kule tunakopaswa kufika. Nawaambia wanachama na mashabiki Yanga hapa siyo mwisho, tumejipanga kumalizia," alisema Kaze.

Mshambuliaji nyota wa timu hiyo ambaye juzi alifunga bao la kwanza na 'assist' ya goli la pili, Fiston Mayele, alisema anaamini wanaweza kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kutokana na kikosi kizuri walichonacho.

Yanga imetinga fainali baada ya ushindi wa jumla wa mabao 4-1 wakati wapinzani wao, USM Alger waliwachapa ASEC Mimosas magoli 2-0, baada ya suluhu ya ugenini.