Mayele, Sakho wampa mzuka Sheva

17May 2023
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mayele, Sakho wampa mzuka Sheva

WINGA na mshambuliaji wa zamani wa Simba, Miraji Athumani 'Sheva', ameelezea furaha yake ya kurejea tena Ligi Kuu akiwa na timu yake mpya ya JKT Tanzania, kwa kuwa alikuwa akitamani kuchezaji ligi moja na straika wa Yanga, Fiston Mayele na winga wa Simba, Pape Sakho.

 

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Miraji ambaye aliichezea Klabu ya Simba mwaka 2019 hadi 2020, alisema ni bahati iliyoje kurejea tena kwenye Ligi Kuu na kwamba ndoto yake ilikuwa kuwa ligi moja na baadhi ya mastaa anaowakubali kwa sasa, Mayele na Sakho.

"Nawakubali wengi, lakini hawa wachezaji wanacheza kwenye nafasi ambayo mimi nacheza na naiga vitu vingi kutoka kwao, mimi ni straika na winga pia, Mayele yeye kosa moja goli moja, Sakho ni msumbufu, mimi pia kuna viti naokota huko, sasa na mimi nimekuja huko huko, nitaonyesha nilichokuwa nacho, kikubwa tu ni kumuomba Mungu nisipate majeraha," alisema Miraji ambaye mashabiki wake wanamwita 'Sheva', wakimfananisha na straika wa zamani wa Chelsea, AC Milan na timu mbalimbali za barani Ulaya, Andriy  Shevchenko.

Akiwa ni mmoja wa wachezaji walioipandisha daraja JKT Tanzania kutoka Ligi ya Championship msimu huu, amethibitisha kubaki kwenye kikosi hicho kwa sababu hajapokea ofa yoyote kutoka timu zingine.

"Safari ya Championship ilikuwa ndefu na ngumu, nilimisi kucheza Ligi Kuu na timu kubwa, timu nzuri ili nionyeshe tena nilichokuwa nacho kwa sababu mashabiki wengi hawajaniona na wamenisahau kwani muda mrefu sikucheza soka kutokana na kuwa majeruhi.

"Nilipata majeraha, nilivunjika mfupa mdogo wa mguu wa kushoto, ndicho kilichosababisha kupotea kwa muda mrefu kwenye ramani ya soka, sasa nimepona, maisha yanaendelea nipo  JKT Tanzania si Simba tena," alisema.

Wakati huo huo, timu ya JKT Tanzania juzi ilikabidhiwa kombe lao la ubingwa wa Championship kwenye mechi maalum iliyochezwa Uwanja wa Uhuru dhidi ya Transit Camp na kutoka sare ya mabao 2-2.