Baada ya juzi kufanikiwa kuvuna pointi tatu dhidi ya Mtibwa Sugar, sasa Polisi Tanzania wanahitaji alama tatu dhidi ya Simba ambao watakutana nao Mei 24 na 28 watamaliza msimi na Azam FC mechi zinazotarajiwa kupigwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Polisi Tanzania iko nafasi ya pili kutoka mkiani ikiwa na pointi 25 na wakifanikiwa kupata alama zote sita katika mechi hizo mbili watakuwa na jumla ya alama 31, ambazo zinaweza kuwatoa kwenye nafasi hiyo kutegemeana tu na kama Mbeya City yenye alama 30, KMC FC pointi 29 sawa na Mtibwa Sugar, zitapoteza mechi zao mbili za mwisho.
Akizungumza na Nipashe jana, Zahera alisema wamejipanga vizuri kuelekea michezo miwili iliyosalia kuhakikisha wanapata pointi sita ili kuinusuru timu hiyo kuendelea kubaki katika ligi hiyo.
Alisema ushindi walioupata katika mechi iliyopita umesaidia wachezaji wake kujiamini na kuendelea kupambana katika mechi mbili zilizosalia kuhakikisha wasaka pointi zote sita ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuepuka kucheza Championship msimu ujao.
“Hatuko kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo, tunatakiwa kupambana kushinda mechi zote zilizosalia kujiweka kwenye nafasi nzuri za kuendelea kusalia Ligi Kuu msimu ujao,”alisema Zahera.
Aliongeza kuwa michezo iliyosalia ni migumu kwa sababu watakuwa ugenini na wachezaji wanatakiwa kupambana kuhakikisha wanafanikiwa kupata alama zote sita.
“Mechi zote mbili tutacheza ugenini, tunakutana na timu ambazo zinahitaji kupata matokeo, lakini na sisi tunahitaji ushindi katika michezo yote hiyo kwa sababu ya hali yetu katika msimamo,” alisema kocha huyo.










