Mkataba wa Azam Media wa miaka mitatu unamalizika mwaka huu na tayari Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa amesema wameanza mchakato kwa ajili ya kupata kituo cha kuonyesha ligi hiyo msimu ujao.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwesigwa alisema tayari kuna vituo kadhaa vimejitokeza kushindana na Azam Media kwa ajili ya kupata haki hiyo katika msimu ujao wa ligi.
"Kuna vituo kadhaa vimejitokeza kushindana na Azam, lakini hakuna kituo kutoka nje ya nchi," alisema Mwesigwa.
Katibu huyo alisema baada ya kukipata kituo wataangalia namna ya kuuboresha mkataba wa awali, ambao ulilalamikiwa na baadhi ya klabu huku, Yanga wakisusia kuchukua mgao wa fedha zilizotolewa kwa klabu zote za ligi kuu na mdhamini (Azam Media).
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga akizungumza jana, alisema kama TFF kupitia bodi ya ligi watashindwa kutatua changamoto za mkataba uliopita, hawatakuwa tayari kusaini.
"Lazima kuwe na tofauti na hili tunaliona kwenye ligi za nje, haiwezekani klabu kubwa kama Yanga kupata mgao sawa na klabu nyingine ndogo," alisema Sanga.










