Pamoja na kufungwa bao 1-0 katika mechi hiyo, wawakilishi hao wa pekee Tanzania wamesonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1.
Katika mechi ya kwanza wiki mbili zilizopita, Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 2-0, Simon Msuva akifunga bao la kwanza kwa kichwa cha mbizi na Anthony Matheo akifunga kwa shuti la mwendo mrefu.
Katika mchezo huo uliojaa kila aina ya ushindani, huku wenyeji wakitawala sehemu kubwa ya mchezo, kipa wa Yanga Deogratius Munishi 'Dida' aliiokoa timu yake baada ya kudaka penalti dakika ya 87.
Kabla ya Dida kuicheza penalti hiyo, beki Nadir Haroub 'Cannavaro' alionyeshwa kadi nyekundu kwa mchezo mbaya.
Katika mchezo huo, bao pekee la wenyeji lilipachikwa kwenye kamba na mchezaji, Love Kabulungu katika dakika ya 25.
Pamoja na kufungwa bao hilo, Yanga ilijituma kutafuta bao la kusawazisha, huku wenyeji wao wakiendeleza mashambulizi kusaka bao lingine.
Mara ya mwisho Yanga kucheza hatua ya makundi ilikuwa wakati wakishiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1998.
Kwa kucheza hatua makundi, wawakilishi hao wa Tanzania watavuna zaidi ya Sh. milioni 600.
Yanga ilihamia katika mashindano hayo na kucheza mechi za mtoano baada ya kutolewa na Al Ahly kwenye raundi ya pili ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika kwa kichapo cha jumla magoli 3-2.
Kiungo Thaban Kamusoko alionyeshwa kadi ya njano mapema kabla wenyeji hawajapata bao la kuongoza na baadaye walianza kucheza mipira ya krosi na kupiga pasi za chini wakijaribu kupenyeza mashambulizi kusaka mabao zaidi.
Dakika ya 64 Kocha Mkuu wa Yanga Hans van der Pluijm alimtoa Kamusoko na nafasi yake kuchukuliwa na Deus Kaseke baada ya kuona nyota huyo anaweza kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
Yanga ndiyo timu pekee ya Tanzania iliyobakia kwenye mashindano ya kimataifa.










