Yanga yaitumia Mamelodi kunasa mbinu za Marumo

09May 2023
Na Waandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Yanga yaitumia Mamelodi kunasa mbinu za Marumo

WAKATI uongozi wa Yanga ukikutana jana kujadili faini ya jumla ya Dola 35,000 za Marekani, ambazo ni zaidi ya Sh. milioni 82 za Tanzania, walizotozwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Kocha Mkuu wa timu hiyo,

Nasreddine Nabi, amesema tayari amepata mbinu za kuivaa Marumo Gallants FC katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kesho.

Yanga kwa sasa ipo kambini ikiendelea na mazoezi kwa ajili ya mchezo wa nusu fainali mkondo wa kwanza dhidi ya Marumo Gallants FC ya Afrika Kusini, utakaopigwa kesho katika Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam majira ya saa 10:00 alasiri, ambapo wapinzani wao hao wakitarajiwa kutua nchini leo alfajiri.

Akizungumza na Nipashe jana, Nabi alisema wanaendelea kufanyia kazi madhaifu na ubora wa wapinzani wao kulingana na walivyowaona juzi wakicheza mchezo wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini dhidi ya Mamelodi Sundowns.

Alisema wameona ubora wa safu yao ya ushambuliaji na ulinzi, na kwamba licha ya wapinzani wao hao kupoteza kwa mabao 2-0 katika mechi yao ya nyumbani ya ligi, wamekuwa na matokeo mazuri katika michuano ya kimataifa.

“Tunaingia katika huu mchezo kwa nidhamu kubwa, tunaenda kucheza na timu nzuri na haitabiriki kwenye michezo yao, na tunatakiwa kucheza kwa tahadhali kubwa kulinda wapinzani wetu wasipate nafasi ya kuwafunga na kuyatumia madhaifu yao ya safu ya ulinzi kumaliza mechi nyumbani kabla ya kwenda Afrika Kusini.

"Tumewafuatilia mechi waliyocheza juzi ya ligi nchini kwao na kufungwa mabao 2-0, hii haitatufanya kuwaona wapinzani wetu ni wabovu kwa sababu wamefanikiwa kufika katika hatua hii ya nusu fainali si timu ya kubezwa,” alisema Nabi.

Aliongeza kuwa malengo yao ni kumaliza mechi hiyo nyumbani, kwa kutoruhusu kufungwa au sare ili watakapokwenda Afrika Kusini kwenye mchezo wa marudiano, wasicheze kwa presha kubwa ya kutafuta matokeo jambo linaloweza kuwasababishia kutolewa mashindanoni.

Aidha, alisema wapo tayari kwa mchezo huo na kazi kubwa wameifanya kwenye mazoezi na sasa ni zamu ya wachezaji wao kuifanya kazi yao na kuwafurahisha mashabiki wao na kuweka heshima ya klabu hiyo juu.

Kuelekea mechi hiyo, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, amewataka mashabiki wao kuonesha nidhamu ya hali ya juu katika mchezo huo na kutotumia miale ya moto (fataki) katika ushangiliaji.

Hiyo ni baada ya Yanga kutozwa faini kwa makosa mbalimbali yanayodaiwa kufanywa katika mechi yao ya robo fainali dhidi ya Rivers United ya Nigeria, iliyochezwa  Aprili 30, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ambapo Rivers walitoa malalamiko yao siku moja kabla ya mechi hiyo baada ya kumaliza mazoezi yao uwanjani hapo.

Rivers United walilalamika gari yao kuvunjwa vioo na kuibiwa dola 5000 huku wakidai pia kupuliziwa dawa, hivyo Kamati ya Maadili ya Caf, iliyokutana Mei 4, mwaka huu, ikaipiga faini Yanga kiasi cha dola 10,000 za Marekani kwa kosa la kuwasha vitochi na kupiga mafataki uwanjani na dola 25,000 kwa madai ya kupuliza dawa kwenye gari la timu ya wapinzani wao huku wakitakiwa kulipa faini hizo ndani ya siku 60 tangu kutolewa kwa adhabu hiyo, lakini pia imetoa nafasi kwa klabu hiyo kukata rufani ndani ya siku tatu.

Kamwe alisema barua hiyo imewafikia na kwamba imeainisha makosa hayo na jana viongozi walitarajiwa kukutana kupitia baada ya hapo watatoa taarifa rasmi.

“Ni kweli barua hiyo kutoka Caf tumeipokea, niwaombe mashabiki wanapokuja uwanjani katika mechi yetu ya Jumatano dhidi ya Marumo Gallants, wasitumie zile fataki ili kulinda klabu yetu maana tayari tumetozwa faini kwa sababu ya mechi iliyopita,” alisema Kamwe.