Kabla ya mchezo huo utakaochezwa katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma Mei 27, mwaka huu wananchi watapata fursa ya kufanya uchunguzi wa awali wa magonjwa yasiyoambukiza kuanzia Mei 25 hadi Mei 28.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dk. Julius Mwaiselage, amesema ugonjwa wa saratani bado ni tatizo nchini huku takwimu za hivi karibuni zikieleza kuwa Tanzania inapata wagonjwa wapya 42,046, kila mwaka.
Amesema saratani ya shingo ya kizazi inaongoza miongoni mwa saratani 10 zinazowashambulia watu nchini ikifuatiwa na saratani ya matiti.
Dk. Mwaiselage ametaja saratani nyingine nane zinazowashambulia watu nchini kuwa ni njia ya chakula kooni, saratani ya kichwani na shingo, kaposi sarcoma, tezi dume, thyroid, utumbo mpana, lymphoma na saratani ya damu.
“Saratani ya matiti imeongezeka sana, ilikuwa namba nne lakini sasa ndiyo inaongoza. Saratani ya tezi dume nayo haikuwamo kwenye hizi 10, lakini sasa ni ya sita,” amesema.
Mwenyekiti wa Machifu Tanzania, Antonia Tomisiza, amesema nia ya mechi hiyo ni kusaidia juhudi za serikali katika kuwahudumia wagonjwa wa saratani.
Amesema: “Tunaomba wananchi, mashirika, kampuni na sekta binafsi kushiriki katika kuchangia matibabu kwa kuwa wagonjwa wengi hawana uwezo,”










