Mechi JKT Queens, Fountain Gate kuamua ubingwa Simba Queens

11May 2023
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mechi JKT Queens, Fountain Gate kuamua ubingwa Simba Queens

HATMA ya Simba Queens kutwaa tena kwa mara ya nne ubingwa wa Tanzania Bara kwa Soka la Wanawake huenda ikajulikana leo wakati JKT Queens itakapokuwa ugenini kuikabili Fountain Gate Princess katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

 

Simba Queens ambayo juzi ilipata ushindi wa mabao 2-0 kwenye uwanja huo huo dhidi ya Baobab Queens, itakuwa ikiombea mechi ya leo imalizike kwa sare au ushindi uende kwa Fountain Gate Princess ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa huo.

Mabao ya juzi ya Simba Queens yalifungwa na Jentrix Shikangwa, straika hatari kutoka Kenya aliyesajiliwa kipindi cha dirisha dogo, ambaye ametimiza jumla ya mabao 16, akiongoza kwenye jedwali la ufungaji, Mrundi Joelle Bukuru akiongeza la pili dakika za mwisho wa mchezo.

Ni matokeo yaliyoipeleka tena kileleni na pointi 42, ikiwa imebakisha mechi moja tu dhidi ya Ceasiaa Queens utakaochezwa kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha Mkwawa Mei 17, mwaka huu.

JKT Queens ina pointi 40, ambapo kama ikishinda zote itafikisha alama 46 na kutwaa umalkia, huku Simba Queens ikimaliza na pointi 45, hivyo sare yoyote au kufungwa ni ahueni kubwa kwa mabingwa hao.

Fountaina Gate Princess nayo ina nafasi ya kutwaa ubingwa kama itashinda mechi ya leo, kwani kwa pointi 38 ilizonazo kama itashinda leo itafikisha alama 41, na mechi ya mwisho ikipata matokeo mazuri itamaliza na pointi 44, huku ikiziombea mabaya timu za Simba Queens na JKT Queens zipoteze michezo yao.

Awali mechi hiyo ilikuwa uchezwe jana, lakini Afisa Mtendaji Mkuu wa Fountain Gate, Augustine Ngamesha alisema wamepata maagizo kutoka Shirikisho la Soka nchini (TFF), kuwa mechi hiyo ipelekwe mbele kwa siku moja kupisha mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Yanga na Marumo Gallants iliyochezwa jana Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.