Azam juzi ilifanikiwa kutinga fainali ya Kombe la Azam Sports Federation, maarufu Kombe la FA baada ya Dube kuifungia bao la ushindi dakika ya 75 akitokea benchi huku akiwa mwiba mkali kwa mabeki wa Simba katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.
Akizungumza na Nipashe jana, Kali alisema kuwa, siri ya Dube kuwatungua Simba ni kutokana na kuwa na njaa ya kufunga magoli huku akitambua mbinu za mabeki wa Simba kwa kuwafuata nyuma kila mara.
"Prince anakuwa na njaa ya magoli, staili yake ya kucheza na aina ya mpira wanaocheza Simba inakuwa nzuri kwake, anapenda kukimbia nyuma ya mabeki wa Simba ambao hawapendi mshambuliaji kukimbia nyuma yao, hivyo ndio maana anawasumbua na kufanya vizuri.
"Ni aina ya mchezaji ambaye huwa hapendi kushindwa ukimpa maelekezo anakwenda kuyafanyia kazi," alisema Kali.
Aidha, akizungumzia mchezo huo aliongeza: "Tumepambana na kufanya vizuri, mechi ya kwanza na Simba na hii zina utofauti mkubwa, hivyo tumeangalia kitu gani kinaweza kutusaidia tushinde na tumekifanyia kazi na tumefanikiwa na tumepata matokeo mazuri, hakuna mazingaombwe, watu wamejituma na kujitoa".
Azam FC ni mara yake ya kwanza kuiondoa Simba katika michuano ya Kombe la FA, kwani mara tatu walizokutana kabla ya juzi, zote Wekundu wa Msimbazi hao waliibuka na ushindi.
Kwa matokeo hayo Azam FC sasa inasubiri mshindi kati ya Yanga na Singida Big Stars katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Liti mkoani Singida Mei 21, mwaka huu, ili kujua timu watakayokutana nayo fainali kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.










