Yanga yaionya Al Ahly kwa Mkapa jumamosi

28Nov 2023
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga yaionya Al Ahly kwa Mkapa jumamosi
  • Yasema inakuja wakati mbaya, huku  ikiweka wazi robo fainali ni lazima, hivyo…

KLABU ya Yanga imesema inataka kuwafuta machozi ya kufungwa mabao 3-0 dhidi ya CR Belouizdad, kwa kushinda mechi yao Jumamosi dhidi ya Mabingwa Watetezi, Al Ahly ya Misri, itakayochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe.

Akizungumza Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema Al Ahly wamekuja wakati mbaya, ambao Yanga wanahitaji furaha kwa udi na uvumba baada ya kupoteza mechi ya kwanza.

“Sisi msimu huu tunaitaka robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, tumeanza kwa kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya CR Belouizdad na hii inakumbusha msimu uliopita, tulianza vibaya kama hivi kwenye Kombe la Shirikisho, tulivyorudi nyumbani, moto halisi wa Yanga ulianza kuonekana kwa hiyo naamini Jumamosi ijayo moto utawaka haijalijalishi anakuja nani.

“Tunajua Al Ahly ni timu kubwa, lakini kuelekea kwenye mechi hii imekuja wakati mbaya ambao Yanga tunahitaji furaha, tumeshatoka kupoteza mechi yetu, hakuna kiswahili Yanga tunataka kufurahi Jumamosi,” alisema Kamwe.

Alisema kikosi cha Yanga haki takuwa na mapumziko yoyote, badala yake kitakwenda moja kwa moja kambini kwa ajili ya mechi hiyo.

“Hakuna muda wa kupumzika kwa sababu wanachama na mashabiki wa Yanga wanachokitaka ni pointi tatu za nyumbani, wanataka furaha, benchi la ufundi na wachezaji wanajua hilo kwa hiyo wameanza kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwa ajili ya mechi hiyo, tunataka pointi tatu za nyumbani,” alisema.

Akizungumzia hali ya kipa wao namba moja raia wa Mali, Djigui Diarra, ambaye hakukaa langoni kutokana na maumivu ya bega, alisema anaendelea vizuri, lakini kukaa au kutokaa langoni katika mechi ya Jumamosi kutategemea ripoti ya madaktari.

“Alikuwa na tatizo la bega na ndiyo maana alikosa mechi dhidi ya Coastal Union, hata alipoenda kwenye majukumu yake ya timu ya taifa hakucheza vile vile, madaktari wamemshauri ni bora akakaa nje kidogo ili apone kwa asilimia 100 kuliko akajilazimisha halafu shida ikawa kubwa zaidi.

“Tupo kwenye Ligi ya Mabingwa kila taarifa huwa ni muhimu, ukiitoa unampa ahueni mpinzani, anajiandaa kutokana na mapungufu ulionayo, benchi la ufundi lilishauri taarifa kama hizi tuzihifadhi ili kutotoa fursa kwa mpinzani kujua taarifa za kiufundi kuelekea kwenye mchezo huu,” Kamwe alifafanua.