WACHEZAJI wa Yanga wanaingia katika mchezo wa hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakiwa wenye furaha baada ya kupewa bonasi nzuri kufuatia kuwafunga mahasimu wao wa jadi, Yanga SC mabao 2-0 Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, mabao ya Donald Ngoma kipindi cha kwanza na Amissi Tambwe kipindi cha pili yalitosha kuifanya Yanga iendeleze ubabe kwa mahasimu wake hao wa jadi.
Na baada ya ushindi huo, uongozi wa Yanga umewapatia bonasi nzuri wachezaji kuwashukuru kwa kuwajengea heshima dhidi ya watani. Hakuna kiongozi wa Yanga aliyekuwa tayari kutaja kiwango cha fedha walichowapa wachezaji wao.
“Mambo kama haya ni siri, kwa sababu wachezaji hawapendi watangaziwe wanachopata kwa kuhofia usumbufu kutoka kwa familia zao,”amesema Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro.
Wakati wachezaji wa Yanga wakiwa wenye furaha, upande wa pili mahasimu wao, Simba hali ni tofauti kidogo. Uongozi chini ya rais Evans Aveva umechukizwa na kipigo hicho na hauna furaha kabisa na wachezaji wake.
“Hatujapewa chochote, hapa tunasubiri mishahara yetu,”amesema mmoja wa wachezaji wa Simba ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini.
“Unajua huwa inauma sana kufungwa mechi na Yanga kwa sababu mnakosa fedha nyingi sana mnazokuwa mmeahidiwa na pia mkifungwa mnatoka mikono mitupu kabisa,”amongeza mchezaji huyo.
Yanga SC ilirejea kileleni mwa Ligi Kuu Jumamosi baada ya kuwachapa 2-0 watani wao, Simba SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mabao ya Mzimbabwe Ngoma kipindi cha kwanza na Mrundi Tambwe kipindi cha pili, hivyo kufikisha pointi 46 baada ya kucheza mechi 19, wakati Simba SC iliyocheza mechi ya 20 leo, inabaki na pointi zake 45 na kushuka hadi nafasi ya tatu.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga SC ivune pointi sita msimu huu kwa watani, baada ya mechi ya mzunguko wa kwanza pia kushinda 2-0 Septemba 26, mwaka jana mabao ya Tambwe kipindi cha kwanza Malimi Busungu kipindi cha pili.
Hii ni mara ya kwanza Yanga inaifunga Simba SC mechi zote za msimu za Ligi Kuu tangu mwaka 1999, msimu ambao Mtibwa Sugar waliibuka mabingwa.
Msimu wa 1999, wakati huo Ligi Kuu inadhaminiwa na bia ya Safari Lager inayotengenezwa na kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Yanga iliichapa Simba 3-1 Mei 1, 1999 mabao ya Idd Moshi, Kali Ongala na Salvatory Edward la wapinzani likifungwa na Juma Amir Maftah, wakati marudiano wana Jangwani wakashinda 2-0 Agosti 29, 1999 mabao ya Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ na Mohamed Hussein 'Mmachinga'.
Na siku hiyo Simba ilicheza pungufu tangu dakika ya 24, baada ya beki wake wa kati, Abdi Banda kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na refa Jonesia Rukyaa wa Kagera kwa kumchezea rafu Ngoma.









