Jeshi latishia kuiondoa Yanga kwenye mashindano

24Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
Lete Raha
Jeshi latishia kuiondoa Yanga kwenye mashindano

KOCHA Mkuu wa JKT Mlale ya Ruvuma, Edgar Msabilila ametamba wataifunga Yanga katika mchezo wa leo wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hatua ya 16 Bora Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

WACHEZAJI WA YANGA

Akizungumza na Lete Raha jana, Msabilila amesema wamejipanga vyema na kikosi chake kipo fiti kucheza na Yanga na wataifunga kutoka na ubora wao, ukilinganisha na upinzani wao ambao wametoka kwenye mechi kubwa na uchovu unaweza ukawapunguza kasi.

Yanga ilikuwa na mechi ngumu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Simba ambayo hata hivyo waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

“Kikosi changu kina wachezaji vijana wasiokuwa na majina makubwa, kwa hivyo watacheza kwa kujituma ili waonekane na kujitangaza, kwa sababu Yanga ni timu kubwa”alisema Msabilila.

Yanga leo inatarajiwa kutumia wachezaji ambao hawana nafasi kwenye kikosi cha kwanza kwenye mechi za Ligi Kuu katika mchezo huo dhidi ya timu hiyo ya Daraja la Kwanza.