Mabingwa hao mara 25 wa Tanzania Bara watashuka kwenye Uwanja wa Taifa Jumamosi kuikabili timu hiyo ya Ligi Kuu ya Mauritius katika mechi ya marudiano ya hatua ya awali ya Klabu Bingwa Afrika.
Tayari Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limewatangaza waamuzi wa Eritrea kuchezesha hiyo huku wageni wa Yanga wakitarajiwa kutua nchini keshokutwa.
Yanga ilishinda kwa bao 1-0 ugenini wiki juzi na inahitaji ushindi au sare ya aina yoyote kusonga mbele.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro, alisema jijini Dar es Salaan jana kuwa kikosi chao kinaendelea vizuri na maandalizi ya mechi hiyo na tayari CAF wamewatumia majina ya waamuzi wa mchezo huo ambao wote wanatokea Eritrea.
"Wapinzani wetu wanataingia nchini Alhamisi tayari kwa mchezo wetu wa Jumamosi, wametutumia taarifa hiyo na sisi tunaendelea na maandalizi ya mwisho mwisho," alisema Muro.
Muro alisema mechi hiyo itachezeshwa na mwamuzi wa kati Amaneal Eyob Ruessom atakayesaidiwa na Hugh Mohamedberhan Abdelkadir na Idris Mohamed Osman huku mwamuzi wa akiba akiwa Suleiman Salih Ali.










