Yanga kanyaga twende

19Mar 2016
Somoe Ng'itu
Dar
Nipashe
Yanga kanyaga twende

YANGA leo ina kazi moja tu ya kulinda ushindi walioupata ugenini watakapoikaribisha APR ya Rwanda katika mechi ya marudiano Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Taifa, dar es Salaam.

yanga.

Mabingwa hao wa Tanzania watakuwa na kibarua kinene cha kulinda utangulizi wa mabao 2-1 waliupata kwenye mechi ya wiki mbili zilizopita kwenye Uwanja wa Amahoro, Kigali, Rwanda.

APR, timu mali ya Jeshi la Rwanda, iliwasili nchini juzi jioni na kutamba kuwa wamekuja kubadilisha matokeo ya mchezo wa awali na kusonga mbele.

Hata hivyo, wanakutana na wenyeji Yanga, ambao ili kusonga mbele hatua inayofuata, wanahitaji sare aina yoyote ingawa Kocha Hans van der Pluijm amesema wanataka ushindi.

Pluijm alisema jana kuwa watashuka uwanjani bila kubweteka na ushindi walioupata Kigali.
"Hatutabweteka, kazi bado haijamalizika, wao (APR) wako Tanzania kutafuta ushindi wakiamini wanaweza kuupata," alisema Pluijm.

Kocha wa APR, Nizar Khanfir hakuzungumza na wanahabari siku kikosi chake kilipowasili nchini, lakini jana alisema wamekuja kuing'oa Yanga kwenye mashindano.

"Tunajua tunaweza kusonga mbele, lakini kwa kuifunga Yanga na kuindoa kwenye mashindano. Tumejiandaa kwa mchezo utakaotupa matokeo mazuri," alisema.

Yanga ilifika hatua hiyo baada ya kuifunga Cercle de Joachim ya Mauritius mabao 3-0, wakati wapinzani wao APR waliwaondoa 'vijana' wa Mfalme Mswati wa Swaziland, Mbabane Swallows kwa kichapo cha 4-2.
Mshindi kwenye mchezo huyo atakumbana na Al Ahly ya Misri au Libolo ya Angola.