Simba yatamba kuwatumbua wababe wa Yanga, Azam

19Mar 2016
Sanula Athanas
Tanga
Nipashe
Simba yatamba kuwatumbua wababe wa Yanga, Azam
  • Timu hiyo ya Msimbazi itaingia kwenye Uwanja wa Mkwakwani leo jioni ikisaka ushindi ili ijitanua kileleni mwa msimamo wa VPL kwa pointi saba.

KOCHA mkuu wa muda wa Simba, Jackson Mayanja, amesema mechi yao ya leo dhidi ya Coastal Union itakuwa ngumu, lakini kikosi chake kimejipanga 'kuwatumbua' wababe hao wa Yanga na Azam FC.

Jackson Mayanja.

Licha ya kuwa mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Coastal Union ambayo Mayanja aliinoa kabla ya kujiunga na Simba Desemba mwaka jana, imeweka rekodi ya kuwa timu pekee iliyoshinda dhidi ya Yanga na Azam msimu huu.

Katika mahojiano na Nipashe akiwa safarini kutoka Dar es Salaam kuja mjini hapa jana mchana, Mayanja alisema anafahamu ugumu wa mtihani alionao leo dhidi ya Wagosi wa Kaya.

"Itakuwa mechi ngumu sana kwetu kesho (leo), Mganda huyo alisema. "Coastal wako katika nafasi mbaya ya kushuka daraja. Pia msimu huu wameshinda dhidi ya Yanga na Azam hapo Tanga, watataka kushinda dhidi ya Simba.

"Sisi (Simba) tunataka kutwaa ubingwa. Tumejipanga kuwakabili. Ni jambo jema hatuna majeruhi kikosini. Tumefanya mazoezi Dar es Salaam leo (jana) asubuhi, wachezaji wako na moyo ya kushinda."

Ally Jangalu, kocha wa Coastal, aliliamba gazeti hili mjini hapa jana mchana kuwa amefanyia kazi upungufu uliojitokeza katika mechi mbili zilizopita walizolala 3-0 dhidi ya Mtibwa Sugar na Kagera Sugar.

Aidha, ofisa habari wa timu hiyo, Oscar Assenga, aliiambia Nipashe mjini hapa jana mchana kuwa mgogoro wa kimaslahi kati ya wachezaji na uongozi wa mabingwa hao wa Tanzania Bara 1988, umetatuliwa na wanaamini "mwendo wa ushindi unaanzia kwa Simba leo".

Simba ambayo iko kileleni mwa msimamo wa ligi ya Bara ikiwa na mtaji wa pointi 54, itaingia kwenye Uwanja wa Mkwakwani ikiwa na kumbukumbu ya kushinda 1-0 dhidi ya kikosi cha Jangalu jijini Dar es Salaam duru la kwanza.

Matokeo ya awali baina ya timu hizo
Coastal 0 1 Simba 2011/12
Coastal 0 0 Simba-2012/13
Coastal 0 0 Simba-2013/14
Coastal 0 0 Simba-2014/15
MECHI ZINGINE LEO
Majimaji vs Mbeya City
Stand United vs Ndanda FC