Yanga fainali bila Mayele, Aziz Ki

13Jun 2023
Adam Fungamwango
TANGA
Nipashe
Yanga fainali bila Mayele, Aziz Ki
  • …Azam yapania kulibeba kombe, Kaze asisitiza hakuna wa kuwazuia lakini…

MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga, leo watashuka uwanjani kujaribu kukamilisha furaha ya msimu kwa kutwaa Kombe la Shirikisho (FA) watakapoumana na Azam FC huku ikikosa huduma za nyota wake, Fiston Mayele na Aziz Ki.

 

Mayele ambaye amekuwa na msimu mzuri atakosekana kwenye mchezo wa leo baada ya kwenda kujiunga na timu yake ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo sawa na Aziz Ki aliyeenda kujiunga na timu yake ya taifa ya Burkina Faso.

Mratibu wa timu hiyo, Hafidh Saleh aliiambia Nipashe jana kuwa licha ya juhudi za uongozi wa timu hiyo kuomba wachezaji hao wacheze mchezo wa leo ndipo waondoke, imeshindikana na kuwalazimu kuwaachia waondoke.

Jamhuri ya Kidemkokrasi ya Congo ya Mayele wanatarajia kucheza na Gabon, Aziz Ki na timu yake ya Burkina Faso watacheza dhidi ya  Cape Verde, mechi zote hizo zitachezwa Juni 18 kuwania kufuzu fainali za Afrika. 

 

Mchezo wa leo ni fainali ya aina yake ambapo Yanga wanataka kukamilisha furaha ya msimu baada ya kutwa taji la Ligi Kuu na kufanikiwa kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika wakisubiri kuona kama watatwaa ubingwa wa FA.

 Yanga itaingia kwenye mechi hiyo ikitaka kulitetea kwa mara ya pili kombe hilo, kwani ililichukua Julai 2, mwaka jana, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha, ilipoifunga Coastal Union kwa mikwaju ya penalti 4-1, baada ya kushuhudia dakika 90 zikienda sare ya mabao 3-3.Hata hivyo, Azam itataka kulichukua kombe hilo baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa miaka mitatu iliyopita, mara ya mwisho ikiwa ni 2019, ilipoifunga Lipuli bao 1-0 la Obrey Chirwa katika mchezo wa fainali Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi.Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze amesema pamoja na kwamba timu zote zimepata nafasi ya kucheza mechi za kimataifa, lakini Yanga ni timu kubwa na kila mechi dhidi ya timu nyingine inakuwa na presha ya mashabiki, hivyo ni lazima wapambane ili kupata ushindi."Tunaingia uwanjani kwa kazi moja ya kusaka ushindi ili tupate kombe la pili msimu huu, tutawapa furaha mashabiki wetu na tumalize msimu wa mashindano vizuri," alisema Kaze.Kocha Msaidizi wa Azam FC, Kally Ongala, alisema timu yake imepitia mambo mengi na mechi ngumu hadi kufikia hapo, na kuongeza kuwa kila mechi ina mfumo wake, hivyo watacheza tofauti na walivyocheza dhidi ya Simba kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo."Kila kitu kipo tayari tumejiandaa na dakika 90 ndizo zitaamua," alisema Ongala na kuongeza,“Ni mechi ambayo timu itakayoshinda tu itatwaa kombe, tayari tuna tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa, lakini kombe hili tunalitaka sana na litakuwa faraja baada ya kukosa ubingwa msimu huu,” alisema Ongala.

Alisema wanaiheshimu Yanga kwa kuwa ndio mabingwa watetezi na mabingwa wa Ligi Kuu lakini kwake ni dakika 90 pekee ndizo zitaamua bingwa wa FA msimu huu.