Robertinho ameutaka uongozi huo kwanza kufanya usajili kwa kufuata kile alichokieleza kwenye ripoti yake ambayo ameikabidhi kwa uongozi wa klabu hiyo.
Nipashe inafahamu maagizo hayo ni juu ya wachezaji anaowataka kusajiliwa na wale ambao ameomba waondolewe kwenye timu kwa kuwa hawatakuwapo kwenye mipango yake msimu ujao.
Mmoja wa wajumbe wa bodi wa klabu hiyo alisema jana jioni walikaa na kuanza kuipitia ripoti ya kocha huyo kwa lengola kuanza kuyafanyia kazi maagizo yake.
“Ni kweli ripoti ya kocha imefika na tumekutana katika kikao maalumu kuipitia na kuanza kuifanyia kazi, bodi imepania kuhakikisha timu inafanya vizuri msimu ujao na ndio maana tupo makini katika mchakato mzima wa usajili na uboreshaji wa kikosi chetu, alisema mjumbe huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Aidha, akizungumza na Nipashe jana mchana, Meneja wa Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alikiri Mbrazil huyo ameondoka kuelekea kwao kwa mapumziko huku akiwaachia majina ya wachezaji ambao hawahitaji kwenye kikosi chake cha msimu ujao.
" Ni kweli mwalimu amerejea kwao kwa ajili ya mapumziko lakini uongozi kwa sasa unajipanga kuanza kushusha vitu kwa ajili ya msimu ujao na hii imetokana na kushindwa kufanya vizuri katika michuano yote ambayo tumeshiriki msimu huu.
" Kikubwa ametuachia ripoti yake na nini ambacho anahitaji kwa ajili ya msimu ujao na kesho Jumatatu (leo) tunatarajia kuweka wazi kwa kuwatangaza nyota ambao tumewapa mkono wa kweli msimu huu," alisema Ahmed.
Aliongeza kuwa uongozi ulikuwa na vikao kwa wiki nzima na kikao cha jana kimehitimisha yale waliyojadili na kukubaliana kama bodi ya klabu.
Vikao hivyo vilikuwa chini ya Mwenyekiti wa Bodi, Salim Abdallah 'Try Again ', na wajumbe wote walihudhuria.










