KMC yatua Mbeya 'kujitafuta' Play Off

13Jun 2023
Na Mwandishi Wetu
MBEYA
Nipashe
KMC yatua Mbeya 'kujitafuta' Play Off

KIKOSI cha timu ya KMC tayari kimewasili jijini Mbeya kwa ajili ya mchezo wao wa kwanza wa mchujo "Play Off' dhidi ya wenyeji Mbeya City utakaopchezwa kesho kwenye Uwanja wa Sokoine.

 

KMC imetua Mbeya ikitokea Sumbawanga ilipoenda kucheza mchezo wao wa mwisho wa ligi kuu dhidi ya wapinzani wao hao ambapo waliibuka na ushindi wa bao 1-0 ushindi ambao hata hivyo haukuwasaidia kukwepa kucheza mchezo huo wa mchujo.

Akizungumza na Nipashe, ofisa habari wa klabu hiyo, Christina Mwagala alisema maandalizi kuelekea mchezo huo yanakwenda vizuri na wachezaji wote wapo katika hali nzuri kuelekea kwenye mchezo huo muhimu.

"Tunafahamu hatupo kwenye hali nzuri kujihakikishia kubaki ligi kuu msimu ujao, mchezo huu ni muhimu na wachezaji wetu wanatambua, kila mmoja akili ameelekeza kwenye mchezo huu kwa sababu hatutaki kushuka daraja," alisema Christina.

Aidha, Christina amewaomba mashabiki wa timu hiyo kuendelea kushirikiana nao katika kipindi hiki kibaya lakini ana imani wao kama KMC watafanikiwa kubaki Ligi Kuu msimu ujao.

KMC imemaliza Ligi Kuu ikiwa katika nafasi ya 13 baada ya kujikusanyia pointi 32 ikiwa ni pointi moja zaidi ya Mbeya City iliyomaliza katika nafasi ya 14.

Timu itakayofungwa kwenye matokeo ya jumla baada ya michezo miwili itashuka daraja moja kwa moja na itakayoshinda itakwenda kumenyana na Mashujaa FC ya ligi daraja la kwanza kuwania kucheza ligi kuu msimu ujao.