Waogeleaji bado wasotea viwango

25Apr 2016
Renatha Msungu
Nipashe
Waogeleaji bado wasotea viwango

LICHA ya Hilal Hilal kupata medali ya shaba katika mashindano ya kimataifa yanayoendelea nchini Mauritius, hakuna muogeleaji wa Kitanzania mpaka sasa ambaye amefuzu kushiriki michezo ya Olimpiki itakayofanyika Agosti jijini Rio de Janeiro Brazil.

Muda unaotakiwa kupata tiketi ya kushiriki michezo ya Olimpiki ni sekunde 23, wakati Hilal alitumia sekunde 24 katika mashindano ya mita 50 waliyoogelea nchini humo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), Ramadhani Namkoveka alisema hali hiyo ya kukosa mwakilishi kwenye michezo hiyo ambayo imefikia ukingoni jana imewaumiza.

"Waogeleaji wetu wanashindwa kutumia muda uliopangwa na FINA (Shirikisho la Kuogelea duniani, hakuna aliyefikiwa viwango kwa sababu wanatumia sekunde 24 au zaidi kila wanapokwenda kwenye mashindano," alisema Namkoveka.

Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, kamati ya utendaji itakutana kwa ajili ya kuona kama waendelee kutafuta mashindano ya kufuzu au wajitoe na kusubiri ofa itakayotolewa na FINA ya kupeleka waogeleaji.

Alisema timu hiyo ilitarajia kuingia jana jioni ikitokea Mauritius ambako ili kutafuta nafasi lakini imerejea mikono mitupu.
Hata hivyo alisema bado kuna nafasi ya kuendelea kushiriki mashindano ya kufuzu hadi Julai 2 mwaka.