Baadhi ya wadau wa soka wamelilaumu jeshi la polisi kwa kushindwa kuwadhibiti mashabiki na kusababisha vurugu hizo zilizomjeruhi vibaya mshika kibendera baada kupigwa jiwe kichwani.
Mwamuzi wa mechi hiyo ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho, Abdallah Kambuzi ililazimika kuimaliza kabla ya muda baada ya mashabiki kurusha mawe na chupa za maji kama kielelezo cha kupinga bao la pili la Yanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Mbali na kulilaumu jeshi la polisi, lakini pia wadau wamesema miundombinu ya Uwanja wa Mkwakwani unaotumika kwa mechi za Ligi Kuu, siyo salama kutokana na kutoa nafasi kwa mashabiki kuingia ndani karibu kabisa na eneo la kuchezea bila kikwazo.
Mkuu wa Kituo cha Tanga, Khalid Mohamed alikiri askari waliohudhuria mchezo huo walizidiwa nguvu na mashabiki.
Akizungumza na gazeti hili jana, mmoja wa viongozi wa Chama cha Soka Wilaya ya Tanga, Swedi Mkwabi alisema hali ya usalama kwenye uwanja huo ilikuwa mbaya.
Alisema idadi ya askari waliokuwapo uwanjani hapo, ishingetosha kuwadhitibi mashabiki waliojazana uwanjani kushuhudia mechi hiyo iliyolazimika kuongezwa dakika 30 baada ya muda wa kawaida dakika 90 kumalizika kwa timu hizo kufungana bao 1-1.
Aidha, Mkwabi aliyewahi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, alisema vurugu hizo zingeweza kuepukwa kama waamuzi wa mechi hiyo wangekuwa makini.
"Ni jambo lililokuwa wazi, walikuwapo uwanjani walishuhudia. Waamuzi walikuwa chanzo cha vurugu, siwezi kusema kwamba walipendelea, lakini hawakuwa makini kutimiza majukumu yao," alisema Mkwabi.
Kwa upande wake, kamisaa wa mchezo huo, Osuri Kosuri kutoka Simiyu alisema ulinzi uwanjani hapo ni kama haukuwepo kabisa.
Alisema askari walishindwa kuwadhibiti mashabiki hivyo kutoa mwanya wa kufanya walivyotaka ikiwa ni pamoja na kurusha mawe na chupa za maji.
"Mwamuzi alikuwa sahihi kuuvunja mchezo kutokana na kukosekana kwa hali ya usalama uwanjani hapo. Hali ilikuwa mbaya sana, nadhani kuna kila sababu ya kuimarishwa usalama kwenye viwanja vya soka," alisema na kuongeza:
"Isingekuwa rahisi mwamuzi kuendelea na mchezo wakati mashabiki walikuwa na nafasi ya kupenya hadi uwanjani bila kikwazo kutoka kwa askari."
Vurugu hizo zilisababisha mwamuzi namba mbili, Charles Simon kupigwa jiwe karibu na jicho na kuumia vibaya uwanjani hapo.
Aidha, usalama kwenye uwanja huo ni mdogo kutokana na ukweli kwamba miundombinu yake inayotenganisha jukwaa na sehemu ya kuchezea kuwa dhaifu.
Nipashe ilishuhudia mashabiki hasa walemavu wakiingia hadi ndani ya uwanja na kukaa jirani na eneo la kucheza, jambo ambalo ni hatari.
Mbali na walemavu kuingia kwenye eneo hilo, lakini pia baadhi ya watu wasiohusika na eneo la ndani ya uwanja wamekuwa wakiingia ovyo bila kudhibitiwa.
Akizungumzia vurugu hizo, kocha wa Mwadui FC, Jamhuri Kiwhelu alisema tukio hilo ni aibu kubwa katika mchezo wa soka.
Alisema kilichofanywa na mashabiki wanaodaiwa kuwa wa Coastal Union ni kibaya kutokana na ukweli kwamba mchezo wa soka siyo vurugu bali furaha.
"Coastal Union hawakupaswa kufanya vurugu, walitakiwa kuendelea na mchezo hata baada ya kufungwa bao la pili, pengine wangeweza kusawazisha bao hilo," alisema kocha huyo ambaye timu yake ilitolewa kwenye mashindano hayo baada ya kufungwa na Azam FC juzi.
Imeandikwa na Somoe Ng'itu (Tanga), Renatha Msungu na Faustine Feliciane (Dar).










