Tambwe ambwaga Kiiza magoli Ligi Kuu

26Apr 2016
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Tambwe ambwaga Kiiza magoli Ligi Kuu

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Amissi Tambwe amembwaga Hamisi Kiiza wa Simba kwa idadi ya mabao ya kufunga tangu waanze kucheza Ligi Kuu Bara.

Wachezaji hao wa kimataifa kutoka Burundi na Uganda, wanapishana bao moja.

Hadi sasa, tayari Tambwe amepachika mabao 51 katika mechi za ligi tangu msimu wa 2013/14 akitoka nchini Burundi, huku Kiiza akitikisha nyavu mara 50 tangu msimu wa 2011/12.

Tambwe amefunga idadi hiyo ya magoli kwa msimu mitatu tu, huku Kiiza akitumia misimu minne kupata idadi hiyo ya magoli.

Rekodi zinaonyesha kuwa Kiiza aliingia nchini kwa kusajiliwa na Yanga 2011 na Tambwe akiletwa na klabu ya Simba mwaka 2013.

Wachezaji hao kwa sasa ni kama wamebadilishana timu, kwani Kiiza yupo Simba na Tambwe Yanga.

Pia rekodi zinaonyesha Tambwe hadi anaondoka Simba akiwa amecheza msimu mmoja na nusu na kufunga mabao 20 mechi za ligi Kuu na hadi sasa ameifungia Yanga magoli 31 ndani ya nusu msimu uliopita.

Kwa upande wa Kiiza, aliondoka akiwa ameifungia Yanga magoli 31, akicheza kwa misimu mitatu, na msimu huu wa kwanza Simba tayari ameshatupia magoli 19.

Hata hivyo kwenye kinyang'anyiro cha kusaka kiatu cha dhahabu, Kiiza na yeye anamzidi Tambwe goli moja akiwa na magoli 19, dhidi ya 18.