Kabla ya kufunga bao la pili la Wanalambalamba katika ushindi wao wa 2-1 dhidi ya Panone FC juzi na kuvuka hatua ya 16-bora ya Kombe la Shirikisho, straika huyo wa kimataifa kutoka Kenya, alikuwa amefunga bao moja tu kwenye mshindano yote msimu huu.
Mchezaji huyo wa zamani wa Tusker FC, Petro Atlético, FK Baku, Hoàng Anh Gia Lai, A.F.C. Leopards na Al-Merreikh, alifunga bao moja, Azam iliposhinda 2-0 dhidi ya Stand United mjini Shinyanga Septemba 16.
Baada ya kufunga goli lake loa kwanza mwaka huu, Wanga alikaririwa jana akieleza kuwa alikuwa analisubiria kwa muda mrefu bao hilo na amelipokea kwa furaha kubwa kutokana na kuiwezesha timu yake kupata ushindi.
"Nafuraha kufunga, ni muda mrefu, nilikuwa na matatizo mengi, labda yakaniathiri kiakili," Wanga alikaririwa kwenye mtandao rasmi wa Azam FC jana.
"Lakini namshukuru Mungu, nawashukuru wachezaji wenzangu, benchi la ufundi na viongozi wote pamoja na mashabiki kwa sapoti wanayonipa, nimeweza kufunga bao nililokuwa nasubiria kwa muda mrefu.
"Ujue, mshambuliaji ukikaa muda mrefu bila kufunga inakuathiri. Nitaendelea kufanya bidii na kufunga zaidi. Ni mara yangu ya kwanza kucheza kwenye kiwanja kama hiki (Ushirika), kimetupatia wakati mgumu."
Wanga (30) alijiunga na Azam FC Julai mwaka jana baada ya kumalizika kwa mkataba wake na Al-Merreikh ya Ligi Kuu ya Sudan.










