Mrisho Mpoto awaangukia Watanzania tuzo za Kora

03Mar 2016
Dar
Nipashe
Mrisho Mpoto awaangukia Watanzania tuzo za Kora

MSANII wa muziki wa asili, Mrisho Mpoto, 'Mjomba', amewaomba Watanzania kumpigia kura ili ashinde katika tuzo za muziki za Kora zitakazofanyika kwenye klabu ya Windhoek Country nchini Namibia Machi 20.

Mrisho Mpoto, 'Mjomba',

Mtaalam huyo wa kughani, ameteuliwa kuwania tuzo hizo katika kipengele cha Msanii Bora wa Muziki wa Asili Afrika akichuana na Mathias Walukaga (Uganda), Stanlux (Togo), N’Dulo Kitoxi (Angola), Kandla Kora (Guinea) na Demba Tandla (Mauritania)

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mpoto alisema anajivunia kupewa fursa hiyo, lakini haitakuwa na maana kama Watanzania watakuwa nyuma kumpigia kura.

"Nawaomba Watanzania mpige kura kwa wingi ili niweze kupata tuzo hiyo, itazidi kuipashia lugha yetu ya asili (Kiswahili)," alisema Mpoto ambaye pia alieleza kuwa anatarajia kuzindua wimbo wake mpya wa 'Sizonje' jijini Dar es Salaam Jumamosi.

Wasanii wengine wa Tanzania waliopenya kwenye tuzo hizo ni Yamoto Band ambao wanawania tuzo ya Msanii Anayechipukia Afrika na Wakazi ambao wameingia katika kipengele cha Msanii Bora wa Afrika - Hip-Hop.

Vanessa Mdee ameingia katika vipengele viwili akichuana na Irene Ntale (Uganda), Victoria Kimani (Kenya), Juliana Kanyomozi (Uganda), Knowless Butera (Rwanda) na Avril Nyambura (Kenya) kulamba tuzo ya Msanii Bora Kike - Afrika Mashariki huku pia akipenya kwenye kipengele cha Kolabo Bora ya Mwaka kupitia wimbo wa ‘Tusimame’ alioshirikiana na Emanuel Jal, Juliana na Syssi Mananga.