Isihaka aitolea uvivu Simba

03Mar 2016
Sanula Athanas
Dar
Nipashe
Isihaka aitolea uvivu Simba
  • Timu hiyo ya Msimbazi imemsimamishwa kwa muda usiojulikana beki huyo huku ikitangaza kumlipa nusu mshahara.

WAKATI kocha wa muda wa Simba, Jackson Mayanga akiupongeza uongozi wa klabu hiyo kwa kumfungia Hassan Isihaka, beki huyo amefunguka kilichotokea na kusababisha kufikiwa kwa hatua huyo.

Hassan Isihaka wa Simba akijaribu kuzuia mpira usitoke nje ya uwanja mbele ya Donald Ngoma wa Yanga.

Jumatatu uongozi wa Simba ulitaka kumfungia mchezaji huyo na kupendekeza alipwe nusu mshahara kutokana na kile ulichodai kuwa utovu wa nidhamu.

Huku akiomba radhi kwa uongozi, Isihaka (21), alisema jana kuwa Mayanja ni sawa na mzazi wake na hakuratajia kukwazana naye alipomfuata kujua hatma ya soka lake.

"Nilimfuata kocha (Mayanja) kupata ufafanuzi wa baadhi ya mambo," Isihaka alisema. "Tumevuka nusu ya msimu, lakini mechi nilizocheza Simba msimu huu ni chache na hii ni hatari kwa soka langu na ninapenda kuwa ninaitwa kwenye timu ya taifa.

"Mayanja ni mwalimu wangu, ni sawa na baba yangu, nilimfuata kwa nia njema, lakini maelezo yangu pengine hakuyapokea vizuri.

"Naomba radhi kama nimemkosea, lakini kama mchezaji anayependa kazi yake nilidhani nilipaswa kuuliza kwanini sipati mechi nafasi ya kucheza. Kama nakosea uwanjani, kwanini siambiwi baada ya mechi?" Alihoji beki huyo.

Isihaka ambaye pia ni nahodha msaidizi wa Simba, alianza kukosa uhakika wa kupangwa kwenye kikosi cha Simba tangu Desemba 19 mwaka jana timu hiyo ilipolazimishwa sare dakika ya 90+3 na Toto Africans kwenye Uwanja wa Kirumba jijini Mwanza.

Baada ya mechi hiyo kumalizika, aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Dylan Kerr aliiambia Nipashe hakufurahishwa na safu yake ya ulinzi siku hiyo huku akiweka wazi kuwa "Isihaka hakutimiza majukumu yake vizuri kutokana na kumwacha mfungaji (Ernest Benard) aruke peke yake na kupiga kichwa mpira wa krosi ya Salum Chuku".

Isihaka hakuwa sehemu ya kikosi cha Kerr katika mechi zote mbili za Ligi Kuu zilizofuata dhidi ya Mwadui mjini Shinyanga (Desemba 26) na Ndanda FC mkoani Mtwara (Januari Mosi) hadi Mwingereza huyo alipofukuzwa Januari 10 baada ya Simba kuvuliwa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi na Mtibwa Sugar.

Baada ya kukabidhiwa mikoba ya Kerr, Mayanja aliendelea kumtumia kiungo Abdi Banda katika nafasi ya Isihaka, jambo ambalo linaonekana kumkera beki huyo.