Yanga yaanika utamu kambi ya pemba

02Mar 2016
Somoe Ng'itu
Dar
Nipashe
Yanga yaanika utamu kambi ya pemba
  • ***Mabingwa hao waliichapa Simba wakitokea kisiwani humo, Jumamosi wanakutana na Azam FC wakitokea huko huko...

KOCHA wa Yanga, Hans van der Pluijm, anajivunia ubora wa kikosi chake kwa sasa, lakini pia ameanika utamu wa kupiga kambi kisiwani Pemba.

Kocha wa Timu ya Yanga Hans Van Der Pluijm, akiwaongoza wachezaji wake kutoka uwanjani baada ya kumaliza kwa mazoezi.

Mabingwa Yanga, waliwafunga wapinzani wao wakubwa Simba mabao 2-0, ushindi walioupata wakitokea kisiwani Pemba.
Jumamosi hii wanakumbana na Azam FC katika mechi kali ya Ligi Kuu Bara mwaka huu na kama kawaida watatokea Pemba.

Akizungumza jana, Pluijm alisema Kisiwa cha Pemba kimetulia na kina sifa na mazingira mazuri ya kuiandaa timu kupata ushindi.

Alisema kisiwa hicho kina hali ya hewa sawa na Dar es Salaam, lakini faida kubwa ni utulivu mkubwa, hali ambayo ni kiini cha kuaindaa timu kufanya vizuri.

"Pemba kuna utulivu wa asilimia 100. Unapojiandaa na mechi kubwa kama hii, wachezaji wanahitaji sehemu tulivu ya kujiandaa," alisema Pluijm.

"Tunapopiga kambi eneo kama hili (Pemba), hakuna mchezaji anayetoka nje ya kambi, kila mmoja anabaki kambini na kufikiria mchezo tu. Hapa ni mahali pazuri kujiandaa na mechi.

Tukiwa Dar es Salaam, foleni za magari ni kubwa, tukienda mazoezini foleni, tukirudi hivyohivyo, lakini hapa Pemba hatufikirii mambo ya foleni."

Yanga yenye rekodi ya kutwaa taji la Ligi Kuu Bara mara 25, inaongoza ikiwa na pointi 46, sawa na wapinzani wao Azam FC, wanaoangukia nafasi ya pili kwa tofauti ya mabao.

Timu hizo kila moja imecheza mechi 19, wakati Simba yenye pointi 45, iko nafasi ya tatu baada ya kucheza mechi 20.
Kuhusu mechi dhidi ya Azam, Pluijm alisema ubora wa washambuliaji kwenye kikosi chake, unampa nafasi ya kushinda mchezo huo wa Jumamosi.

Alisema muungano ushambuliaji wa wachezaji Donald Ngoma na Amissi Tambwe umezidi kuimarika.
"Wachezaji hawa wana njaa ya kufunga mabao, haishangazi kuwaona wakitikisa nyavu karibu kila mchezo. Hii inaonyesha kuwa wanachezaji kwa maelewamo," alisema.

"Mechi itakuwa na ushindani, timu zote zinasaka ushindi ili kujiweka kwenye nafasi nzuri kileleni mwa msimamo, naamini kikosi changu kitafanya vizuri, ingawa siwadharau wapinzani wetu," alisema Pluijm.

Ili kuhakikisha wanashinda mechi hiyo, kocha huyo raia wa Uholanzi alisema ameongeza dozi ya mazoezi.
"Hakuna majeruhi mpya, (Nadir Haroub) Cannavaro anaendelea vizuri na nafasi yake ya kucheza au kutocheza itajulikana Ijumaa, kila mchezaji anaonyesha bidii kwenye mazoezi," alisema kocha huyo.

Daktari wa Yanga, Nassor Matuzya alisema kikosi kina wawili, ambao ni Cannavaro na Salum Telela.