UMISSETA Copa Coca Cola kuibua vipaji


17May 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
UMISSETA Copa Coca Cola kuibua vipaji


SERIKALI imesema itaendelea kuwekeza kwenye michezo kuanzia ngazi za chini kwa vile inaamini ndiko kwenye utajiri wa vipaji.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI) George Simbachawene


Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI) George Simbachawene katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadick wakati wa ufunguzi wa udhamini wa kampuni ya Coca Cola kwenye michezo ya UMISSETA.

Uzinduzi huo ulifanyika kwenye viwanja vya Chuo cha Ushirika, Moshi mwishoni mwa wiki iliyopita.
Simbachawene alisema udhamini wa kampuni hiyo ni moja ya maboresho ya michuano hiyo, ambayo anaamini itasaidia kukuza vipaji.


Alisema mashindano ya UMISSETA ngazi ya taifa mwaka huu yamepangwa kufanyika jijini Mwanza.
"Mashindano ya UMISSETA yamesaidia sana kudumisha umoja wetu wa kitaifa, kuwajengea afya njema wanafunzi, akili, kujenga nidhamu, ukakamavu, kuinua taaluma na kuimarisha ushirikiano," alisema Simbachawene.


Aliwataja baadhi ya wanamichezo waliolipatia taifa heshima, ambao vipaji vyao viliibuliwa kwenye mashindano haya kuwa ni Mrisho Ngassa, Mbwana Samatta, Juma Kaseja, Edibily Lunyamila na mchezaji wa mpira wa Kikapu Hashim Thabeet.


Pia Simbachawene alizielekeza halmashauri za wilaya, miji, majiji na Manispaa kuwa na shule moja ya msingi na sekondari kwa ajili ya kufundisha michezo kwa lengo la kuibua vipaji.


Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Masoko Coca Cola wa Kiwanda cha Bonite, Christopher Loiruk alisema UMISSETA kimekuwa chombo muhimu cha kukuza ichezo katika shule za skondari.


"Ninayo furaha kutangaza rasmi umoja huu kati ya UMISSETA na Coca Cola kushirikiana kufanya mashindano haya kuwa bora kabisa," alisema.


Hii itakuwa mara ya kwanza Coca Cola kudhamini michuano hiyo ambayo wanaamini yataibua vipaji vya wachezaji chipukizi.