Ngoma na Kamusoko walikuwa nje wakitumikia adhabu ya kadi mbili za njano wakati Yanga iliposhinda mabao 2-0 katika mechi ya kwanza iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Kocha wa Yanga Hans van der Pluijm alisema wakati kikosi hicho kinasafiri kuwa kurejea kwa wachezaji hao wawili wa kimataifa kutakiongezea nguvu kikosi chake ambacho kinawania rekodi ya kutinga hatua ya makundi.
Pluijm alisema uwepo wa nyota hao 'utawachanganya' wapinzani wao ambao hawajawaona wakicheza.
"Uwepo wao utaongeza kitu ukilinganisha na mchezo wetu wa kwanza, tunakwenda Angola kupambana na kulinda ushindi wetu tulioupata nyumbani, hawakuwaona Ngoma na Kamusoko tulipokutana katika mechi ya kwanza, hii ni faida kwetu," alisema Pluijm.
Kocha huyo alisema kuwa licha ya kuwa pamoja kuwa faida ya magoli mawili, leo watashuka uwanjani kwa tahadhari ili kuendeleza ushindi katika mchezo huo unaotarajiwa kufanyika kuanzia saa 11:00 jioni kwa saa za Tanzania.
"Hatutacheza kwa kujilinda muda wote wa mchezo, tutahakikisha tunakuwa makini kuwazuia wasipate goli na sisi tutapanga mashambulizi na kua tunatumia vizuri kila nafasi tutakayoipata,' alisema Pluijm.
Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' alisema kuwa wanakwenda Angola kusaka ushindi ambao utawajengea heshima Watanzania wote na si klabu yao pekee.
"Tunaiwakilisha nchi, ushindi na mafanikio tutakayopata yatakuwa ni matunda kwa nchi na si Yanga peke yetu, sisi ni wawakilishi wa Tanzania kwenye mashindano haya," Cannavaro alisema.
Licha ya kukutana na 'mizengwe', kikosi cha Yanga kilitua salama mjini Dundo juzi usiku baada ya kutua kwa usafiri ndege jijini Luanda.
Katika mechi ya kwanza, Simon Msuva na Anthony Matheo ndiyo waliifungia timu hiyo mabao katika mechi hiyo ya mtoano baada ya kutolewa kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika na Al Ahly ya Misri kwa jumla ya magoli 3-2.










