Mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 18 hadi Julai 2 mwakahuu.
Akizungumza kwa njia ya simu jana kutoka Nairobi, Kenya, Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye alisema kuwa Zanzibar ilishindwa kufikia malengo ya kutafuta fedha kutoka kwa wadhamini wa ndani kwa ajili ya kusaidia michuano hiyo.
Musonye alisema tayari sekretarieti ya mashindano hayo itakutana Dar es Salaam wiki ijayo kwa ajili ya kuendelea na maandalizi ya michuano hiyo ambayo mwaka huu itashirikisha timu 13.
"Mwaka huu hakutakuwa na timu kutoka nje ya Cecafa, nchi wanachama wa Cecafa tu ndiyo watachuana na Tanzania Bara itatoa timu tatu, tulishawahi kufanya hivyo kwa Tanzania na Kigali (Rwanda) mwenyeji kuwa na timu zaidi ya mbili," alisema Musonye.
Rais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Ravia Idarous aliliambia gazeti hili kuwa wao ndiyo waliiandikia barua Cecafa ya kuwaeleza kwamba hawawezi kuandaa michuano hiyo kutokana na kukosa fedha za kuhudumia timu.
Ravia alisema ili waandae michuano hiyo, ZFA ilitakiwa kuwa na Sh. milioni 600 jambo ambalo wameshindwa kuzipata.
Timu zinazotarajiwa kushiriki michuano hiyo kutoka Tanzania Bara ni pamoja na mabingwa watetezi wa Kombe la Kagame, Azam FC, Yanga na Simba zote za jijini.










