MWALI HUYU HAPA

15May 2016
Lasteck Alfred
Dar es Salaam
Lete Raha
MWALI HUYU HAPA

MABINGWA wapya wa ligi kuu Tanzania bara timu ya Yanga wamekabidhiwa kombe la ubingwa jana licha ya kutoka sare ya magoli 2-2 dhidi ya wenyeji Ndanda FC kwenye mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mgeni rasmi katika mchezo huo Waziri wa Kilimo, Ufugaji na Uvuvi, Mwigulu Nchemba (MB) ambaye pia ni shabiki mkubwa wa mabingwa hao waliotetea ubingwa wao baada ya kuunyakua msimu uliopita ingawa ni ubingwa wa 26 kwa timu hiyo.

Waziri Mwigulu ndiye aliekabidhi Kombe hill kwa nahodha wa Yanga Nadir Haroub "Cannavaro" na timu ya Yanga
Mechi hiyo ilianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu lakini Ndanda ndiyo walikuwa wa kwanza kupata goli dakika ya 29 kwa mkwaju wa penalti, bao lililofungwa na Omari Mponda baada ya Juma Abdul kumchezea madhambi Atupele Green katika eneo la hatari.

Iliwachukua Yanga dakika sita pekee kurudisha goli hilo kupitia kwa Simon Msuva baada ya kupokea krosi safi ya Geofrey Mwashiuya upande wa kushoto.

Yanga walipata goli la pili kupitia kwa Donald Ngoma dakika ya 40 baada ya kupokea krosi upande ule ule wa kushoto iliyopigiwa na beki Mwinyi Haji.

Kipindi cha pili Mabingwa Yanga waliendelea kulisakama lango la Ndanda lakini wachezaji wao walikosa ubunifu wanaposogelea lango huku mlinda mlango Jackson Chove akiwa makini muda wote.

Salum Minely aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Burhan Rashidi aliisawazishia Ndanda dakika ya 80 baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Atupele Green na kumpita mlinda mlango Deogratius Munishi 'Dida'.

Katika hatua nyingine Mwamuzi wa kati wa Jana Seleman Kimagani alitoa kadi za njano kama adhabu kwa wachezaji wa Ndanda; Nahodha Kigi Makasi dakika 26 na Aziz Sibo dakika ya 49. Kwa upande wa Yanga waliodhibiwa kwa kadi ya njano alikuwa ni beki Kelvin Yondani pekee.

Kikosi cha Yanga kilikuwa; Deogratius Munishi, Juma Abdul, Mwinyi Haji/ Oscar Joshua (dk45), Kelvin Yondani, Vicent Bossou, Thaban Kamusoko,Haruna Niyonzima /Mbuyu Twite (dk 85) Simon Msuva, Amissi Tambwe, Donald Ngoma/Matheo Antony (dk 74), Geofrey Mwashiuya.

Kikosi cha Ndanda; Jackson Chove, Aziz Sibo, Kigi Makasi, Kasian Ponera, Riphat Hamis/ Ahmed Msumi (dk 45) , Hemed Khoja, Willian Lucian, Braison Raphael, Omary Mponda, Atupele Green, Buruhani Rashid/Salum Minely (dk 40)