Mashali amdunda Maarab kwa pointi

16May 2016
Renatha Msungu
Dar es Salaam
Nipashe
Mashali amdunda Maarab kwa pointi

BONDIA Thomas Mashali amefanikiwa kutwaa mkanda wa ubingwa wa Super Middle dhidi ya mpinzani wake Sanjat Maarabu kutoka Iran kwa pointi katika pambano lililofanyika juzi usiki kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa jijini Dar es Salaam.

bondia Thomas Mashali

Pambano hilo lililokuwa na vuta nikuvute lakini Mashali alionekana kumzidi mbinu mpinzani wake na hatimaye kupata pointi nyingi kutoka kwa majaji wawili kati ya watatu waliosimamia.

Jaji wa kwanza Robert Kasanga alimpatia Mashali pointi 115-113, wakati Aga Peter 'Mnazaret' alitoa pointi 116-112 na Said Chaku akimmpa Maarab pointi 116-112.

Akitangaza matokeo hayo Katibu wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa nchini (PST), Anthony Ruta alisema kwa matokeo hayo Mashali aliibuka mshindi wa pambano hilo la kimataifa.

Mtanzania mwingine Saleh Kalekwa alifanikishwa kumdunda James Onyango kutoka Kenya kwa pointi katika raundi ya 10 na kutwaa mkanda wa WBO.

Hata hivyo PST walishindwa kutoa ufafanuzi kuhusiana na kutofanyika kwa pambano lingine la kimataifa kati ya Cosmas Cheka na mpinzani wake aliyetarajiwa kuja nchini akitokea Afrika Kusini.