Bao pekee lililoipa Tanzania ubingwa wa mashindano hayo lilifungwa na Winifrida Gerald dakika ya 41 katika mechi iliyokuwa na ushindani dhidi ya Uganda iliyomaliza katika nafasi ya pili.
Shime alisema kupitia mashindano ya CECAFA U-18, wachezaji wake chipukizi wamepata uzoefu wa mechi za kimataifa na ataendelea na programu mbalimbali kwa ajili ya kuwaendeleza na kuwajenga.
“Hii michuano imekuwa na mwendelezo mzuri kwa timu zetu kwa ajili ya kujiandaa na michuano iliyopo mbele yetu, malengo yetu ni kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia ya mwaka 2027, ninaimani tutafanikiwa,” alisema Shime.
Naye Rais wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Wallace Karia, amesema amefurahishwa na ushindani mkubwa wa soka la wanawake ulioonyeshwa katika mashindano yaliyomalizika Dar es Salaam juzi.
Karia alisema wanachama wa CECAFA wanatakiwa kuendelea kuwalea na kuwalinda wachezaji vijana kwa ajili ya matayarisho ya michezo ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2027.
Alisema mashindano yalikuwa magumu hadi hatua ya mwisho hakuna nchi ambayo ilikuwa na uhakika wa kutwaa ubingwa kati ya Tanzania na Uganda ambazo zilipata ushindi katika michezo yake mitatu iliyotangulia.
Aliongeza taswira inaonyesha soka la wanawake Tanzania limepiga hatua kubwa na sasa ni tishio katika ukanda huu.
“Hawa wasichana tunatakiwa kuwalea vizuri na kuwatunza kwa sababu ya kuwatayarisha kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia 2027.
"Kwa timu za Zanzibar, tunafanya jitihada kubwa ya kuhakikisha wanapata mechi nyingi za kirafiki kwa ngazi ya Taifa kwa sababu kuna wachezaji wazuri na wenye uwezo wa kusaidia timu katika mashindano hayo ya 2027,” alisema Karia.
Aliongeza licha ya timu chache kushiriki, mashindano hayo yamefanikiwa kwa asilimia kubwa.










