Azam FC juzi iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Bandari FC ya Mombasa, shukrani kwa Prince Dube na Cheikh Tidiane Sidibe, waliocheka na nyavu katika mechi hiyo.
Akizungumza na Nipashe baada ya mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Dabo alisema licha ya kushinda hajafurahishwa na kiwango cha vijana wake kama alivyotegemea.
Alisema wamepata ushindi, lakini hana furaha na matokeo hayo kutokana na makosa kadhaa ya kiufundi ambayo yalifanywa na wachezaji wake kwenye mchezo huo.
“Matokeo si muhimu sana, nahitaji kuangalia timu yangu inafanya nini, tumeshinda lakini sina furaha, tulikuwa na makosa kadhaa hatari kwetu kama ilivyotokea kwenye michezo mingine.
"Lakini pia tuna baadhi ya matukio tulifanya vizuri ila bado tuna kazi ya kufanya ili tuwe kwenye ubora ule tunaoutaka, kabla ya Agosti 9, mwaka huu katika mchezo wetu wa Ngao ya Jamii,” alisema Dabo.
Kocha huyo alisema anaendelea kufanyia kazi mapungufu yao ili kujiimarisha haraka kwa sababu mipango yao mikubwa ni kuanza vizuri katika Ngao ya Jamii kwa kutwaa taji hilo.









