Akizungumza jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe alisema kikosi chao kitaondoka Jumatatu kwa ndege kwenda Tanga na kitafika siku hiyo na kupata mapumziko, kabla ya kufanya mazoezi Jumatano.
"Kikosi kitaelekea Tanga Jumatatu, tutakuwa na siku moja ya mazoezi siku ya Jumanne na, Jumatano ndiyo tutacheza pambano letu dhidi ya Azam FC," alisema Kamwe.
Kamwe alisema benchi la ufundi chini ya kocha Miguel Gamondi amewahakikishia wanaenda kufuata taji hilo la Ngao ya jamii na kurudi nayo Dar es salaam.
"Kila kitu kipo sawa, benchi la ufundi limetuambia kikosi kipo tayari sasa kuifuata ngao yetu, tunaenda Tanga kuendeleza furaha yetu pale tulipoishia msimu uliopita," alisema Kamwe.
Aidha, aliwataka wanachama na mashabiki wa klabu hiyo mikoa ya Pwani, Kilimanjaro na Arusha kufurika kwa wingi uwajani ili kuwapa hamasa wachezaji ambao watakuwa wanaanza kazi ya kutetea mataji yao waliyoyapata msimu uliopita.
"Niwaambie wanachama na mashabiki wa Yanga wa mikoa ya jirani na Tanga wajitokeze kwa wingi, Jumatano ni siku yetu ya kwenda kuujaza uwanja wa Mkwakwani, waje wawape sapoti wachezaji wao," alisema Kamwe.
Alisema kikosi chao kipo tayari kwa ajili ya mikikimikiki ya meimu mpya na michezo hiyo ya Ngao ya jamii ni ufunguzi kuelekea kwenye ligi itakayoanza Agosti 15
Yanga itacheza mechi ya Ngao ya Jamii Jumatano ijayo dhidi ya Azam FC kabla ya siku ya Alhamisi, Simba kushuka uwanjani hapo dhidi ya Singida Fountaine Gate.
Mshindi wa kila mchezo watakutana kwenye fainali kuwania taji hilo kwa msimu huu.










