Mechi hiyo pekee kwenye ratiba ya ligi leo, itapigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kabla ya matokeo ya mechi nyingine za mwisho wa wiki hii, Simba ilikuwa kileleni kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 56, na Azam katika nafasi ya pili wakiwa na pointi 55.
Iwapo Simba wataondoka na ushindi leo, basi watafikisha pointi 60 na kuendelea kuongoza msimamo huku nyuma wakiacha presha Yanga na Azam, ambazo ni washindani wa karibu wa mbio za ubingwa.
Hiyo ina maana kwamba, ushindi kwa Simba leo wataendelea kubaki kileleni mwa msimamo, huku ligi ikiendelea kusogea hatua za lala salama.
Kocha wa Simba, Jackson Mayanja anafahamu kuwa kikosi chake hakihitaji matokeo mengine yoytote zaidi ya yale yatakayowapa pointi tatu.
Baada ya kufungwa na kutupwa nje ya michuano ya Kombe la Shirikisho hivyo kukosa nafasi ya kucheza michuano ya Afrika mwakani, Simba sasa inaelekez nguvu zote kusaka ubingwa wa Bara.
Hata hivyo, Wekundu hao wa Msimbazi watakuwa na kazi ngumu ya kuwazuia Toto Africans, kwani pamoja na kuwa salama kwenye msimamo wa ligi, hawatataka kupoteza mchezo huo.
Kocha John Tegete anafahamu kuwa kikosi chake kinachezaji dhidi ya timu inayosaka ubingwa, hivyo amewaandaa wachezaji wake kucheza 'jihadi'.










