Kwa ushindi huo, kikosi cha kocha mkuu wa muda, Mganda Jackson Mayanja, kimefikisha pointi 54 baada ya mechi 23, pointi nne mbele ya Yanga katika nafasi ya pili, lakini Wanajangwani wana mechi mbili za viporo.
Mabingwa hao mara 18 wa Tanzania Bara, walilazimika kusubiri hadi dakika ya 87 kupata goli hilo muhimu lililofungwa na kiungo mtokeabenchini, Awadh Juma akifumua shuti kali la mguu wa kulia akiwa hatua moja kutoka kwenye boksi la Prisons baada ya kupewa pasi na kiungo mwenzake Jonas Mkude.
Kikosi cha Wanamsimbazi kilitengeneza nafasi nyingi, lakini ubora wa kipa Beno Kakolanya na safu ya ulinzi ya Prisons ulikuwa kikwazo kwa washambuliaji Hamisi Kiiza na Ibrahim Ajibu.
Kwa ushindi huo, Simba ililipa kisasi cha kutunguliwa bao 1-0 na Wajelajela hao katika mechi yao ya duru la kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya Oktoba 21 mwaka jana.
Katika mechi zingine za Ligi Kuu Tanzania Bara jana, Mgambo JKT ilitoka sare ya 1-1 dhidi ya Mwadui FC kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, wakati Kagera Sugar ikiendelea kulizimisha jahazi la Coastal Union kwa kuwachapa mabao 3-0 mjini Shinyanga, huku Majimaji FC wakishinda 1 - 0 dhidi ya Stand United mjini Songea.
Vikosi kwenye Uwanja wa Taifa vilikuwa:
Simba: Vincent Angban, Hassan Kessy, Mohammed Hussein, Novaty Lufunga, Juuko Murshid, Justice Majabvi/ Awadh Juma (dk 70), Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, Ibrahim Ajibu, Hamisi Kiiza/Paul Kiongera (dk 83) na Mussa Mgosi/Daniel Lyanga (dk46).
Prisons: Beno Kakolanya, Salum Kimenya, James Mwasota, Lugano Mwangama, Laurian Mpalile, Jumanne Elfadhil, Lambarti Sabiyanka, Juma Seif ‘Kijiko’/Freddy Chudu (dk 60), Mohamed Mkopi, Jeremiah Juma na Benjamin Asukile.
Imeandikwa na Renatha Msungu na Sanula Athanas










