Tenga rais wa heshima TFF

14Mar 2016
Somoe Ng'itu
Tanga
Nipashe
Tenga rais wa heshima TFF

ALIYEKUWA Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga, ameteuliwa kuwa rais wa heshima wa shirikisho hilo na wajumbe wa mkutano mkuu waliokutana jana jijini hapa.

Aliyekuwa Rais TFF, Leodegar Tenga (Kushoto) akiwa na Rais wa sasa Jamal Malinzi.

Jamal Malinzi, Rais wa sasa wa TFF, aliwasilisha jina la Tenga katika mkutano huo ili wajumbe kulipigia kura na kutokana na mchango wa kiongozi huyo katika maendeleo ya soka nchini, alipitishwa bila kupingwa.

Malinzi alisema kamati ya utendaji ilifikia uamuzi wa kuliwasilisha jina la Tenga kutokana na kuheshimu na kuthamini mchango wake katika soka tangu alipokuwa mchezaji na kiongozi kwenye ngazi mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.

Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam, DRFA, Almassy Kasongo, alitoa sifa za Tenga na kueleza kuwa ameiwakilisha vyema Tanzania ndani na nje ya nchi kwa kiwango cha kimataifa.

Kasongo alisema kuwa mbali na kuiongoza Taifa Stars katika fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 1980 Lagos, Nigeria, Tenga akiwa Rais wa TFF aliweka misingi mizuri ya utawala bora.

Rais huyo wa heshima aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Rais wa Baraza la Vyama vya Soka Tanzania (Cecafa) na sasa ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf). Tenga pia aliwahi kuzichezea Yanga na Pan African zote za Dar es Salaam.