Simba chini ya kocha mkuu huyo wa muda, inapambana kuhakikisha inamaliza ukame wa miaka minne bila taji la Ligi Kuu na sasa iko kileleni mwa msimamo wa ligi ya Bara ikiwa pointi nne mbele ya Yanga wanaokamata nafasi ya pili.
Baada ya juzi kufanikiwa kulipa kisasi cha kipigo cha bao 1-0 walichopewa na Prisons Oktoba 21 kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, kikosi cha Mayanja sasa kimeanza maandalizi shadidi kuhakikisha kinashinda dhidi ya Coastal Union ambao msimu huu wamekuwa tishio kwa timu 'vigogo' zinapokanyaga Tanga.
Mabingwa hao wa Tanzania Bara 1988 (Coastal) waliitandika Yanga mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani Januari 30 kabla ya kuibamiza na Azam FC bao 1-0 uwanjani hapo siku 15 baadaye.
Na Mayanja anajua kwamba Wagosi wa Kaya watahitaji "kujenga heshima kwa kuwapiga vigogo". Mganda huyo aliiambia Nipashe jana kuwa nyota wake wanatakiwa kuwa makini katika mechi hiyo.
"Kilichotusadia jana (juzi) ni kucheza kwa kasi na kwa kujituma hadi dakika ya mwisho," alisema. "Tunapaswa kufanya hivyo na ikiwezekana kuongeza nguvu zaidi katika mechi ijayo (dhidi ya Coastal Union) kama kweli tunahitaji kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi.
"Coastal ni timu ngumu, kikosi chetu pia ni kizuri na nimekiandaa kushinda mechi hiyo ya ugenini. Simba ya sasa ni tofauti na niliyoikuta."
Timu hiyo ya Msimbazi imekusanya pointi 54 katika mechi 23 zilizopita ikifuatwa na Yanga wenye pointi 50 baada ya mechi 21.
Kikosi cha Wanamsimbazi kitaondoka Dar es Salaam kwenda Tanga Jumatano kwa ajili ya mechi hiyo.
CITY YAGONGWA TANGA
Katika mechi pekee ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa jana, African Sports wqalifanikiwa kuondoka mkiani mwa msimamo wa ligi hiyo baada ya kuichapa Mbeya City FC mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Mabao yote yalifungwa na straika Omary Issa katika dakika ya 57 na 64 na kuipaisha African Sports kwa nafasi moja hadi ya 15 kwenye msimamo wa ligi.










