Simba imetoka, kombe letu -Julio

13Apr 2016
Adam Fungamwango
Dar
Nipashe
Simba imetoka, kombe letu -Julio

KOCHA mkuu wa Mwadui FC Jamhuri Kihwelo Julio amesema kuwa kama timu ya Simba imetolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, basi ana uhakika kuwa timu yake ndiyo itakayotwaa ubingwa na kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.

kocha mkuu wa Mwadui FC, Jamhuri Kihwelo Julio.

Akizungumzia matokeo ya mechi ya robo fainali kati ya Wekundu wa Msimbazi dhidi ya Coastal Union, Julio alisema timu aliyokuwa akiihofia ni Simba, ambayo sasa haipo tena.

"Mimi nilikuwa naihofia Simba tu kwenye michuano. Simba ndiyo timu pekee yenye wachezaji waliojaliwa vipaji. Sasa kwa sababu imetolewa, naamini taji ni langu (Mwadui)," alisema Julio.

Alisema hazihofii timu zilizobaki kwenye mashindano hayo kutokana na ukweli kwamba hazitishi. "Yanga, Coastal, Azam hazina shida kwetu, tunazimudu vizuri," alisema.

Akizungumzia pambano lenyewe lililochezwa Jumatatu, Julio alisema kuwa tatizo la wachezaji wa Simba walikuwa wakicheza kwa kutaka kufurahisha zaidi mashabiki, wakidhani ni mechi kama ya ligi.

"Mechi kama hizi mfumo wake wa uchezaji ni tofauti na ligi. Hizi ni mechi za mtoano, unachotakiwa wewe ni kucheza ili kupata magoli tu na si vinginevyo, sasa Simba hawatofautishi kati ya mechi za ligi na za mtoano," alisema.
Aliisifu Coastal Union kwa kufahamu aina ya uchezaji kwenye michuano kama hiyo na kupata ushindi.