Simba ilinyukwa 2-1 na Union na kutupwa nje ya michuano ya Kombe la Shirikisho, ambayo bingwa wake anaiwakilisha nchi kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Wakati Mayanja akiwaangushia lawama wanandinga wake, kocha wa Coastal Union, Ally Jangalu kipigo walichopata Simba kilistahil kwa sababu walishuka dimbani wakiwa na kapu la dharau dhidi ya timu yake.
Jangalu alisema, siku hiyo Simba walistahili kipigo cha mabao 3-1 kutokana na walivyotawala mchezo mwanzo mwisho.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mayanja alisema wachezaji waandamizi ndiyo waliokuwa kiini cha kushindwa mchezo huo.
Mayanja alilalamikia utovu wa nidhamu ulioonyeshwa na nyota wake wawili raia wa Uganda, Juuko Mursheed na Hamis Kiiza.
"Hawa ni wachezaji muhimu kwenye timu, kitendo cha kuchelewa kuja kujiunga na timu wakitokea kwenye michezo ya timu ya Taifa ni tatizo," alisema Mayanja.
"Hawajafanya mazoezi na wenzao na kutokana na hilo isingekuwa rahisi kwao kucheza." alisema Mayanja.
Alisema kama timu hiyo ingekuwa imekamilika wa wachezaji wake wote wa kikosi cha kwanza kucheza matokeo yangekuwa tofauti.
Katika mchezo huo, ukuta wa Simba uliokuwa chini ya Hassan Isihaka na Novatus Lufunga ulishindwa kwenda sambamba na kasi ya washambuliaji wa Coastal Union wakiongozwa na Ali Ahmed 'Shiboli' na kujikuata mabeki wa Simba wakicheza faulo mara kwa mara.
Kocha wa Coastal, Jangalu alisema: "Timu nyingi zimekuwa zikitudharau kwa sababu tu tunashika mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara," alisema na kuongeza: "Simba waliingia uwanjani wakiamini kuwa jina lao kubwa ni kama tayari wameshapata ushindi."
Alisema sasa wanajipanga kwa ajili hatua ya nusu fainali na anaamini kikosi chake kitasonga mbele kwenye michuano hiyo.
Kauli ya Simba kiidharau Coastal Union iliungwa mkono pia na mshambuliaji wa timu hiyo ya Tanga, Ally Ahmed 'Shiboli'.
Akizumgumza baada ya mechi kumalizika, Shiboli - mchezaji wa zamani wa Simba, ilikosea ilipoingia uwanjani ikiwa na matokeo ya ushindi kabla hata mechi kuchezwa.
"Simba ni timu nzuri, ila ilijiamini mno. Kama ingeingia uwanjani ikiwa na lengo moja kuwa inakwenda kucheza na timu iliyokamilika, kazi ingekuwa ngumu kwetu, lakini wao waliona wanangia kucheza na timu mbovu. Hilo liliwaponza," alisema Shiboli.
Imeandikwa na Renatha Msungu, Adam Fungamwango na Faustine Feliciane










