Safari ya viporo Yanga, Azam kuendelea leo

13Apr 2016
Somoe Ng'itu
Dar
Nipashe
Safari ya viporo Yanga, Azam kuendelea leo
  • ***Timu hizo zinazoshika nafasi ya pili na tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara zinashuka kwenye viwanja tofauti kucheza mechi zao za viporo...

YANGA na Azam hakuna mapumziko baada ya kupeperusha bendera ya nchi kwenye mashindano ya klabu Afrika wiki iliyopita, Dar es Salaam.

yanga wakifanya mazoezi.

Yanga ilikuwa ikitibuana na Al Ahly ya Misri - Klabu Bingwa Afrika na kutoka sare 1-1 na Azam ilitunishiana msuli na Esperance ya Tunisia na wageni kulala 2-1.

Siku sita baadaye, timu hizo zinageukia mechi za viporo Ligi Kuu Bara leo kwa mabingwa watetezi Yanga kucheza dhidi ya Yanga Mwadui FC kwenye Uwanja wa Taifa.

Azam watasafiri kwenda kuwavaa wabishi wasiofungika kirahisi, Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.

Yanga itashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya sare ya 2-2 katika mechi ya duru la kwanza Oktoba 28 ugenini
Shinyana, wakati Azam ilipata pointi tatu katika mechi ya kwanza kwa ushindi wa 1-0 Desemba mwaka jana.

Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm alisema wamesahau waliyokutana nayo mwenye mechi dhidi ya Al Ahly na sasa wanaelekeza nguvu Ligi Kuu Bara.

"Tunajiimarisha ili tufanye vizuri katika kila mechi. Michuano yote tunayoshiriki tunataka kutwaa taji, hivyo hakuna mchezo mwepesi kwetu," alisema Pluijm.

Akiizungumzia mechi hiyo, Kocha wa Mwadui, Jamhuri Kihwelu 'Julio', alianza kwa kuikosoa timu yake akisema: "Nina bahati mbaya, timu yangu inapocheza vizuri inakosa ushindi, lakini inapoonyesha soka bovu ndio inapata ushindi."

Hata hivyo, alitamba kwa kusema pamoja na mchezo wao dhidi ya Yanga kuwa mgumu, wamejipanga kuhakikisha wanaibuna na ushindi.

"Mechi itakuwa ngumu kwetu na kwa Yanga pia, kila upande unataka kuendeleza ushindi. Kama Yanga walishindwa kutufunga mzunguko wa kwanza, ina maana tunaweza kuwafunga safari hii," Julio alisema.

Yanga imefanya vizuri kwa kushinda kiporo chake cha kwanza dhidi ya Kagera Sugar kwa kushinda 3-1 wakati Azam FC ikitoka sare mara mbili mfululizo dhidi ya Toto Africans (1-1) na Ndanda FC (2-2).

Kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime, alisema jana kuwa wako tayari kwa mchezo huo na dhamira yao ni kushinda ili kulipa kisasi cha kufungwa mchezo wa kwanza.

"Tunaanza na Azam kesho (leo) na Jumamosi dhidi ya Yanga. Tuko imara na Dante (Andrew Vicent) amesharejea kikosini," alisema beki huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars.

Simba inaongoza Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 57 wakifuatiwa na Yanga yenye pointi 53, huku Azam FC ikishika nafasi ya tatu kwa pointi.