Azam wapania kuishangaza Esperance kwao

13Apr 2016
Faustine Feliciane
Dar
Nipashe
Azam wapania kuishangaza Esperance kwao

NAHODHA wa Azam FC, John Bocco, amesema kuwa watawashangaza wapinzani wao kwenye michuano ya kombe la Shirikisho Afrika, Esperance ya Tunisia kwenye mchezo wa marudiano utakaochezwa wiki ijayo.

naodha wa Azam FC, John Bocco.

Akizungumza jana, Bocco alisema ushindi wa goli 2-1 walioupata kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Chamazi, utakuwa nguzo ya wao kufanya vizuri kwenye mechi ya marudiano.

"Tunafahamu mambo yatakuwa magumu kwa sababu watacheza kwenye uwanja wao wa nyumbani, ila tutapambana ndani ya uwanja kuhakikisha tunasonga mbele," alisema Bocco.

Bocco alisema kuwa wamejipanga vizuri kisaikolojia kuepuka hujuma za waarabu ugenini.
"Tufahamu Waarabu wana fitina nyingi ndani na nje ya uwanja wanapocheza nyumbani, tunalifahamu hilo na tutakuwa makini nao."

Wakati huohuo, kikosi cha Azam FC kitaondoka nchini Jumamosi kuelekea Tunisia kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidi ya Esperance utakaochezwa Aprili 19 mjini Tunis.

Katika mechi ya kwanza iliyofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Azam Complex, wenyeji walishinda mabao 2-1 kupitia kwa Farid Mussa na Ramadhani Singano 'Messi'.

Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa Habari wa timu hiyo, Jaffer Iddi alisema maandalizi ya safari hiyo yamekamilika na msafara wao utawahusisha wachezaji wote.

Iddi alisema kuwa leo watacheza kwa tahadhari mechi yao ya Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar lakini wakijipanga kupata ushindi ili kuendeleza mbio za kusaka ubingwa wa Bara.