Simba, Ihefu kibaruani FA

07Apr 2023
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, Ihefu kibaruani FA

MASHINDANO ya Kombe la FA yanatarajiwa kuendelea tena leo kwa Wekundu wa Msimbazi kushuka kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kuwakaribisha Ihefu SC kutoka Mbarali, Mbeya.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally.

Mechi hiyo imeondolewa kwenye Uwanja wa Uhuru uliokuwa utumike awali kutokana na kuwa na matumizi mengine.

Itakuwa ni mechi ya tatu ya robo fainali ya mashindano hayo, baada ya Singida Big Stars na Azam FC kufanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ambayo bingwa hupata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Singida Big Stars iliitwanga Mbeya City mabao 4-1, na Azam FC ikaisulubu Mbeya City magoli 2-0, mechi iliyochezwa Azam Complex.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, aliliambia gazeti hili jana mechi hiyo itakuwa ngumu kutokana na kikosi cha Ihefu kuundwa na wachezaji wengi wakongwe na wazoefu.

"Ihefu ni timu nzuri, ilichokuwa inakosa ni muunganiko, lakini sasa ina wachezaji wazuri wenye uwezo, ndiyo maana iliweza kuzifunga timu zote za Dar es Salaam zilizokwenda kule, Yanga, Azam na KMC, kwa maana hiyo sisi tutaingia kwa tahadhari, lakini pia tunataka tuwaonyeshe sisi ni wakubwa," alisema Ahmed.

Ihefu itaingia katika mchezo huo ikiwa imepunguzwa nguvu kutokana na wachezaji wao Wanigeria, Victor Akpan na Nelson Okwa, kutocheza kwa sababu ya  makubaliano ya timu zote mbili wakati wanapeana nyota hao.

"Akpan na Okwa ni wachezaji wetu ambao wapo Ihefu kwa mkopo na katika makubaliano yetu hawatacheza kwenye mechi yoyote ambayo wao watacheza dhidi yetu," alisema Ahmed.

Alisema Simba iliamua kuwapeleka kwa mkopo nyota hao wawili, wote raia wa Nigeria baada ya kuonekana hawana nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Wekundu wa Msimbazi.

Naye Kocha Msaidizi wa Ihefu, Zuberi Katwila, alisema wamewaandaa wachezaji wao vyema kuelekea mechi hiyo na anaamini watavuna matokeo bora.

Katwila alisema nyota wao wako kamili kiufundi na kisaikolojia kukutana na Simba na kutamba 'wembe' waliotumia kuwanyoa Yanga na Azam huenda pia ukawageukia Simba.

Baada ya mechi ya leo, Simba itasafiri kuifuta Ihefu katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa Aprili 10, mwaka huu kwenye Uwanja wa Highland Estates ulioko Mbarali.