Simba inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika itakutana na Waarabu wa Morocco, Wydad Casablanca na itaanzia nyumbani Aprili 21 na 23, mwaka huu na wataenda kurudiana wiki moja baadaye wakati Yanga inayochuana katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika itakutana na Rivers United ya Nigeria.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliviera 'Robertinho' alisema hakuna mchezo mwepesi katika mashindano ya Ligi yaMabingwa Afrika na hasa ikifika hatua ya robo fainali.
Robertinho alisema kikosi chake kiko tayari kupambana na Waarabu hao na anaamini wachezaji wanafahamu malengo ya kusonga mbele ya timu yao.
"Sio mechi rahisi, tunatakiwa kujipanga na kutumia mechi tunazocheza za nyumbani kujiweka vizuri kwa ajili ya maandalizi ya mechi yetu hiyo dhidi ya Waydad ambao ni mabingwa watetezi," alisema Robertinho na aliongeza;
Kwanini tusiende nusu fainali kama tunajipanga vizuri, wachezaji wakiwa makini na kufuata maelekezo tuliyowapa, ninaimani kubwa ya kombinesheni ya wachezaji akiwamo Chama (Clatous), Saido (Ntibazonkiza)," alisema kocha huyo.
Aliongeza kabla ya mechi yao dhidi ya Wydad, watakuwa na mechi tatu mkononi za nyumbani ambazo zote anahitaji kupata matokeo mazuri.
"Baada ya mechi hizo tutacheza mechi yetu ya dabi dhidi ya Yanga, pia tunahitaji kupata ushindi na kutumia michezo yote hiyo kufanyia kazi makosa yao ikiwamo mashambulizi ya kushtukiza, ikiwa ni maandalizi ya kuwakabili Wydad hapa nyumbani," alisema kocha huyo.
Aliongeza ni faida kubwa kuanza kucheza nyumbani kwa sababu wanahitaji kutumia vizuri uwanja wa nyumbani kwa kutafuta ushindi katika mechi hiyo kabla ya kwenda kumalizia majukumu ugenini.
"Tumepangiwa mpinzani mgumu, nikisema mgumu nina maana halisi ya ugumu, ni timu ambayo imetuzidi kwa kila kitu, kuna dakika 90 za soka ambazo mara nyingi huwa hazijali sana hilo, badala yake zinaangalia timu imejipanga vipi kwa mchezo husika na kama sisi tutajipanga vizuri, kumbuka miaka 20 iliyopita Simba iliwatoa mabingwa watetezi wa Kombe la Afrika (Zamalek), wakiwa kwao, enzi za kina, Juma Kaseja, tunataka kurudia historia ile," alisema Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally.
Naye Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze, alisema wanawafahamu wapinzani wao vizuri na anaimani timu zote zilizofika hatua ya robo fainali ni nzuri lakini sasa rasmi wanaanza kujiandaa kuwakabili Rivers United.
Kaze alisema watakuwa makini zaidi katika mechi zote mbili kwa sababu wanakutana na timu ambayo msimu uliopita iliwaondoa katika mashindano hayo ya CAF.
"Ninaimani Rivers United ya sasa sio ile tuliyokutana nayo mwaka jana, itakuwa timu tofauti, tunaamini sisi wenyewe tunauwezo kupambana kufanya vizuri katika michezo yote miwili kwa sababu tunataka kusonga mbele," alisema Kaze.
Rais wa Yanga, Hersi Said, alisema klabu imeongeza kitita cha bonasi kwa wachezaji wa timu hiyo endapo watasonga mbele katika michuano hiyo ya kombe la Shirikisho Afrika.
Hersi alisema baada ya kumfahamu mpinzani wao sasa wanatarajia kufanya kikao na benchi la ufundi kwa ajili ya kuweka mipango kuelekea mechi hiyo ili malengo yao ya kutinga nusu fainali ambayo kila Mwanayanga anahitaji kuona yatimie.
"Tumefurahi kupangwa na Rivers United, naomba niwahakikishie Wanayanga, tutawapiga kwao Nigeria na hapa nyumbani tutawapiga," alisema Hersi.
Mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele, alisema sasa wanaenda kulipa kisasi katika mechi hiyo.
"Tuliowasubiri tumekutana nao, tunaenda kulipa kisasi, mwaka jana walituondoa, sasa tunarudi uwanjani kufanyia kazi madhaifu yetu kwa ajili ya mechi hiyo, hatutarudia makosa," alisema Mayele.
Imeandikwa na Adam Fungamwango na Saada Akida.










