Yanga itashuka dimbani katika mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu ya kukutana na ushindani kwenye mchezo wa msimu uliopita katika michuano hayo ambao walilazimika kusonga mbele kwa ushindi wa matuta.
Mechi hiyo imepangwa kufanyika kuanzia saa 2:00 usiku na mshindi wa mchezo huo atakutana na Singida Big Stars katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.
Winga machachari Mghana, Bernard Morrison, ameandaliwa kuongoza mashambulizi katika mchezo huo baada ya kuwa nje kwa muda mrefu akipambania hali yake ya majeruhi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, alisema maandalizi kuelekea mchezo huo yamekamilika na wachezaji wake wako tayari kupambana kusaka ushindi na kusonga mbele katika mashindano hayo.
Nabi alisema mechi hiyo itakuwa ngumu kwa sababu wanakutana mara nyingine na Geita Gold ambayo imezidi kuimarika na iliwapa upinzani walipokutana katika mchezo uliopita.
"Kutakuwa na mabadiliko katika kikosi changu kulingana na maandalizi tuliyoyafanya, nitawapa nafasi ya kupumzika wale waliotumika sana, tutacheza kwa nidhamu kubwa kwa sababu Geita Gold FC haitakuja kama ilivyokuwa kwenye mchezo uliopita.
Malengo yetu ni kuvuka katika hii hatua na kucheza nusu fainali, baadaye kutetea ubingwa wetu, lazima mchezo wa kesho (leo), tucheze kwa tahadhari kubwa na kusaka ushindi,” alisema Nabi.
Aliongeza Geita Gold FC si timu ya kubeza hasa katika hatua waliyofikia kwa sababu msimu uliopita iliwasumbua mpaka ikawapeleka kwenye hatua ya matuta.
Kocha Msaidizi wa Geita Gold FC, Mathias Wandiba, alisema wachezaji wao wako fiti na wamejiandaa vizuri kwa mchezo huo isipokuwa Juma Luizio ambaye anaendelea na matibabu.
Wandiba alisema benchi la ufundi na wachezaji wanatambua malengo ya kuvuka hatua waliyofikia, hivyo wamejipanga kuonyesha kiwango kizuri katika mechi hiyo.
“Ni mechi tunayokutana na timu iliyo bora na imeimarika, ikizingatiwa siku chache zilizopita tulipoteza dhidi yao katika ligi, lakini hiyo haijalishi kwa sababu tunakwenda kucheza mechi nyingine na mashindano mengine. Naamini vijana wameshajua ratiba iko vipi," alisema Wandiba.
Mshindi wa mashindano hayo atapata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania Bara katika michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.










