Alikuwa ni yule yule, Prince Dube ambaye amekuwa akiwafunga mara zote msimu huu kwenye Ligi Kuu, akiwafunga tena kwenye mechi ya Kombe la FA.
Dube aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Idris Mbombo, alipachika bao la pili dakika ya 76 baada ya uzembe wa mabeki wa Simba kushindwa kukaba mpira na njia.
Ayoub Lyanga ambaye alikuwa kwenye kiwango cha hali ya juu jana, akaupiga mpira kichwa na Dube akakimbia akifukuzana na mabeki kwenye wingi ya kulia na kuupiga kiufundi kwa juu, mpira huo ukakatika na kujaa wavuni, ukiwaacha walinzi na kipa wao Ally Salim hawana la kufanya.
Straika huyo aliyewatanguliza Azam kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga kwenye fainali ya kombe hilo, aliifunga Simba bao kwenye mechi ya Ligi Kuu mzunguko wa kwanza Oktoba 27 mwaka jana, akafunga tena bao pekee dakika ya 35, Azam ikishinda 1-0, na mechi ya mzunguko wa pili iliyochezwa Februari 21, mwaka huu alipachika bao sekunde ya 15, mechi ambayo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Kiungo mkabaji Sadio Kanoute ambaye aliipatia Simba bao la kufutia machozi, alioneshwa kadi nyekundu dakika nne kabla ya mechi kumalizika na mwamuzi Tatu Malongo kutoka Tanga kwa kumchezea madhambi James Akaminko wakati tayari ana kadi ya njano.
Katika mchezo huo, Simba ilianza mapema kulitia msukosuko lango la Azam kwenye dakika ya tatu tu ya mchezo, baada ya faulo ya Clatous Chama iliyokuwa ikielekea wavuni kupanguliwa na kipa Iddrisu Abdulai na kusababisha purukushani kwenye lango, lakini mabeki wakafanikiwa kufagia hatari hiyo.
Kosa lililofanywa na Joash Onyango dakika ya 11, kuukosa mpira wa kichwa, ulimpa nafasi Idris Mbombo kuuchukua pembeni kidogo mwa uwanja na kupiga krosi iliyoleta kizaazaa kwenye lango la Simba, kabla haujatolewa na kuwa kona.
Kona hiyo iliyopigwa dakika hiyo hiyo, nusura izae bao, kwani uliunganishwa kichwa na Mbombo, mpira ukagonga nguzo ya pembeni na Mohamed Hussein 'Tshabalala' akauondoa kwenye hatari.
Shuti kali la Kanoute lilikwenda nje kidogo ya lango dakika ya 16, alipomegewa pande safi kutoka kwa Saido Ntibazonkiza.
Baada ya kosakosa nyingi, hatimaye Azam iliandika bao la kwanza dakika ya 23 lililowekwa wavuni na beki wa kulia, Lusajo Mwaikenda kwa shuti kali la karibu, akiufumua mpira uliotemwa na kipa Ally Salim.
Ulikuwa ni mpira wa faulo iliyopigwa na Ayoub Lyanga, baada ya kufanyiwa madhambi na Shomari Kapombe, shuti lake lilitemwa na kipa Salim, lisababisha patashika nguo kuchanika langoni, kabla ya mfungaji kuukwamisha wavuni.
Simba ilisawazisha bao hilo dakika tano baadaye, Kanoute akiruka juu kuliko mabeki na kipa wa Azam, akaukwamishwa mpira wavuni kwa kichwa.
Aliunganisha mpira wa faulo uliopigwa na Ntibanzonkiza, kutokana na Kibu Denis kufanyiwa madhambi na Brice Kangwa.
Chama alikosa mabao mawili, dakika ya 32 na 45 ambayo kama angetumia nafasi vizuri, Simba ingeweza kwenda mapumziko ikiwa na mabao matatu.
Kipindi cha pili, Azam iliingia tofauti na kuutawala mchezo kwa kiasi kikubwa na kuwanyima nafasi wachezaji wa Simba kukaa na mpira.
Kuumia kwa Mbombo na kuingia Dube ndiko kulikowaumiza Simba kwani hakuchukua muda mrefu kuuweka mpira ndani ya wavu.
Kocha Roberto Oliveira, alilazimika kuwatoa Jean Baleke na Kibu Denis, nafasi zao kuchukuliwa na John Bocco na Pape Sakho, lakini hali ilikuwa ngumu.
Nafasi pekee kubwa iliyoipata Simba ilikuwa ni dakika mbili kabla mechi kumalizika, Bocco alipoachia shuti kali la mbali, lililotemwa na kipa Iddrisu.
Kuna dalili zote za Simba kukosa kila kitu msimu huu, kwani baada ya kutolewa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Wydad Athletic Club ya Casablanca Morocco, Simba haina matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya sare ya bao 1-1 kwenye mechi iliyochezwa Jumatano iliyopita dhidi ya Namungo na sasa imelikosa Kombe la FA.
Azam sasa inasubiri mshindi kati ya Yanga dhidi ya Singida Big Stars kwa ajili ya fainali itakayochezwa Uwanja wa Mkwakwani Tanga.










